Watu 30 wauawa katika mashambulizi ya wanamgambo nchini Ethiopia
Watu wasiopungua 30 wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo waliobeba silaha katika eneo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa Ethiopia.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Desalegn Chane, kiongozi wa chama kipya cha upinzani cha National Movement of Amhara (NAMA) na kuongeza kuwa, miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi hayo yaliyofanyika baina ya Septemba 6 na 13 ni wanawake na watoto wadogo.
Kinara huyo wa upinzani amesema, "wakulima na jamaa zao walitekwa nyara na kisha wakapelekwa katika shule moja katika eneo la Metakal wakiwa wamepigwa pingu mikononi, na kisha wakauawa mmoja baada ya mwingine kwa kupigwa risasi."
Wimbi hili jipya la mashambulio ya wanamgambo limetia doa katika uongozi wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ambaye anapigania kuleta mageuzi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Watu 29 waliokuwa wameshikwa mateka katika eneo la Benishangul-Gumuz wameachiwa huru. Waliofanya mashambulizi hayo ni katika makundi yanayotaka kukwamisha safari ya mageuzi.

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Ethiopia imesema katika taarifa kuwa, 'kumekuwepo na angalau duru mbili za mauaji ya raia, huku mamia ya wakazi wakifurushwa kutoka makwao.'
Mwezi Juni mwaka jana, raia 50 waliuawa katika shambulizi jingine la wabeba silaha walioukuwa wamevalia magwanda ya kijeshi katika eneo hilo ambalo lipo mpakani mwa Ethiopia na Sudan