Watu milioni moja waathiriwa na mafuriko nchini Ethiopia
(last modified Thu, 01 Oct 2020 07:50:53 GMT )
Oct 01, 2020 07:50 UTC
  • Watu milioni moja waathiriwa na mafuriko nchini Ethiopia

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa watu milioni moja wameathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Ethiopia, ambapo laki tatu miongoni mwao wamelazimika kuyahama makazi yao.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeeleza kuwa, mvua kubwa zinazonyesha katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika zimesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kuwafanya watu takriban lakini tatu kuhama makazi yao tangu mwezi Juni mwaka huu hadi sasa.

Aidha taarifa hiyo imesema walioathirika zaidi na majanga hayo ya kimaukbile ni wakazi wa majimbo ya Afar, Oromiya, Gambella, Kusini, Somalia na Amhara, huku ikionya kuwa, mafuriko hayo pia yameharibu taasisi za afya na kumekuwa na uhaba wa dawa.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, mazingira machafu yaliyosababishwa na mafuriko hayo yameongeza hatari ya kukithiri kwa maambukizi ya virusi vya corona na ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.

Gari lililosombwa na mafuriko.

Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema dola milioni 40 zinahitajika kwa ajili ya kuwafikishia misaada wahanga wa mafuriko hayo hasa chakula, dawa na nyumba za kuwasitiri.

Mbali na Ethiopia, nchi nyingine kadhaa za Afrika zikiwemo Niger, Sudan, Burkina Faso na Senegal zimekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha tangu mwezi Juni mwaka huu, ambapo mamia wameaga dunia.