Rais wa zamani wa Tunisia aikosoa vikali Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64483-rais_wa_zamani_wa_tunisia_aikosoa_vikali_jumuiya_ya_nchi_za_kiarabu
Rais wa zamani wa Tunisia Muhammad Moncef al-Marzouki amekosoa vikali kimya cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na kutolaani kwake mwenendo wa baadhi ya nchi za jumuiya hiyo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2020 07:04 UTC
  • Rais wa zamani wa Tunisia aikosoa vikali Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Rais wa zamani wa Tunisia Muhammad Moncef al-Marzouki amekosoa vikali kimya cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na kutolaani kwake mwenendo wa baadhi ya nchi za jumuiya hiyo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Rais huyo wa zamani wa Tunisia amesema kuwa, Jumuiya ya Nchi za Kirabu imefikia mwisho wake kutokana na hatua yake ya kutopinga mwenendo wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utwala ghasibu wa Israel.

Moncef al-Marzouki ameashiria hali ya sasa ya nchi za Kiarabu na kueleza kwamba, baadhi ya nchi za Kiarabu zimo katika kusambaratika na baadhi ya nyingine zimeingia katika mkumbo wa kuufuata moja kwa moja utawala vamizi wa Israel a Marekani.

Kiongozi huyo wa zamani wa Tunisia ameashiria pia msimamo wa sasa wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kutangaza kuwa, kiwiliwili kinachojulikana kwa jina la Jumuiya ya Nchi za Kirabu hivi sasa kinatoa harufu mbaya baada ya kufa.

Rais wa zamani wa Tunisia Muhammad Moncef al-Marzouki

 

Aidha katika ujumbe wake kwa wakazi wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina, rais wa zamani wa Tunisia amewaambia, hakuna chaguo jengine mbele yenu ghairi ya muqawama na mapambano dhidi ya utawala vamizi wa Israel na hamna budi kuendeleza njia hii.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni viongozi wa Marekani, Sudan na utawala haramu wa Israel walitangaza katika taarifa yao pamoja juu ya kufikiwa makubaliano baina ya Tel-Aviv na Khartoum ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.

Sudan imekuwa nchi ya tatu ya Kiarabu baada ya Imarati na Bahrain kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, hatua ambayo imeendelea kulalamikiwa ndani ya Sudan kwenyewe na hata nje ya nchi hiyo.