Nov 19, 2020 06:58 UTC
  • UNHCR: Maelfu ya Waethiopia wanaendelea kuelekea Sudan

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, vita vinavyoendela katika eneo la Tigray baina ya jeshi la serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) vimewalazimisha raia karibu elfu 30 kukimbilia nchi jirani ya Sudan.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa imesema kuwa, maelfu ya raia wa eneo la Tigray wamelazimika kukimbia makazi yao na kutahadahrisha kwamba mgogoro na maafa makubwa ya binadamu yanatokea sasa nchini Ethiopia.  

Jana Jumatano vikosi vya jeshi la Ethiopia viliripotiwa kusonga mbele kuelekea Mekele, mji mkuu wa jimbo la Tigray, licha ya wito wa kimataifa wa kuanza mazungumzo kati ya Addis Ababa na mamlaka ya eneo hili linalotaka kujitenga ili kumaliza mzozo ambao unaendelea kwa muda wa wiki mbili.

Tigray, Ethiopia

Kusonga mbele huko kwa jeshi la serikali ya Ethiopia kunafanyika baada ya Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia kutangaza kuwa, muhula wa siku tatu uliokuwa umetolewa kwa ajili ya waasi wa eneo la Tigray kuweka chini silaha umemalizika na kuonya kuwa sasa jeshi la taifa litaendelea na operesheni yake ya kuukomboa mji mkuu wa eneo hilo Mekelle, kutoka mikononi mwa waasi.

Jeshi la Ethiopia tarehe 4 mwezi huu wa Novemba lilianza mashambulizi dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)). Hujuma hiyo ilianza kwa amri ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Tags