Moncef Marzouki: Tawala za Kiarabu hazijaanzisha uhusiano na Israel bali 'zimejisalimisha'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64756-moncef_marzouki_tawala_za_kiarabu_hazijaanzisha_uhusiano_na_israel_bali_'zimejisalimisha'
Mohamed Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia amesema kuwa, ni kosa kusema kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, bali lililo sahihi na ambalo ndio ukweli wa mambo ni kuwa, mataifa hayo yamejisalimisha kwa utawala huo vamizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 21, 2020 04:32 UTC
  • Moncef Marzouki: Tawala za Kiarabu hazijaanzisha uhusiano na Israel bali 'zimejisalimisha'

Mohamed Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia amesema kuwa, ni kosa kusema kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, bali lililo sahihi na ambalo ndio ukweli wa mambo ni kuwa, mataifa hayo yamejisalimisha kwa utawala huo vamizi.

Rais huyo wa zamani amekosoa vikali hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kujisalimisha kwa utawala dhalimu wa Israel na kusisitiza kwamba, kuna ulazima kwa mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu kuheshimu haki za taifa la Palestina.

Aidha Moncef Marzouki amesema kuwa, hatua zozote zile ziwe ni za Mamlaka ya Ndania ya Palestina au mataifa mengine ya Kiarabu za kutaka kufikia mapatano na utawala dhalimu wa Israel ni kuzihadaa fikra za waliowengi ulimwenguni.

Kadhalika Bwana Marzouki amesisitiza kuwa: Tunataka amani na mapatano ambayo yatahitimisha machungu na masaibu ya Wapalestina sambamba na kuondoa mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza na sio kujisalimisha kwa utawala ghasibu wa Israe.

Maandamano ya kupinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

 

Tarehe 23 ya mwezi uliopita wa Oktoba, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan ilitangaza kuwa serikali ya mpito ya nchi hiyo imeafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na hivyo kuifanya Sudan nchi ya tano baada ya Misri (1979), Jordan (1994), Imarati na Bahrain (2020) kufikia mapatano na Israel na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa kizayuni.

Kufuatia kutangazwa uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Sudan yamepinga vikali makubaliano hayo, vikiwemo vyama washirika katika muungano unaotawala nchi hiyo.