Kenya kufunga kambi za wakimbizi kutokana na sababu za kiusalama
Kenya imesema inatathmini kufunga kambi zote za wakimbizi nchini humo zikiwemo za Dadaab na Kakuma zenye idadi kubwa ya raia wa Somalia hivi karibuni.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Ndani Karanja Kibicho amesema serikali ya Nairobi imechukua uamuzi huo kutokana na changamoto za kiuchumi na kiusalama na haswa mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara. Kibicho amesema kambi hizo zimechangia pakubwa kushuhudiwa wimbi la mashambulizi ya kigaidi nchini humo na hususan kutoka kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao yake makuu katika nchi jirani ya Somalia.
Kadhalika taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imeongeza kuwa, kutokana na mwendo wa kinyonga wa kuwarejesha wakimbizi hao katika nchi zao chini ya makubaliano ya pande tatu yaani Kenya, Somalia na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, serikali ya Nairobi imeona ni vyema kufunga kambi hizo kwa kuwa imeshindwa kumudu mahitaji ya kila siku ya wakimbizi hao.
Katika kufanikisha mpango huo wa kufunga kambi hizo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imefutilia mbali Idara ya Masuala ya Wakimbizi huku ikiitaka jamii ya kimataifa kuisaidia katika kufanikisha azma yake hiyo.
Kwa sasa Kenya ni mwenyeji wa wakimbizi zaidi ya laki 6 haswa katika kambi za Dadaab na Kakuma ambao wamekuwa nchini kwa takriban robo karne.