Macron: Ufaransa haitaiomba radhi Algeria kwa dhulma za enzi za ukoloni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65920-macron_ufaransa_haitaiomba_radhi_algeria_kwa_dhulma_za_enzi_za_ukoloni
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi hiyo ya Ulaya 'haitatubu' wala kuiomba radhi Algeria kutokana na jinai zilizofanywa na Wafaransa katika zama walipoikoloni nchi hiyo ya Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 21, 2021 00:57 UTC
  • Macron: Ufaransa haitaiomba radhi Algeria kwa dhulma za enzi za ukoloni

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi hiyo ya Ulaya 'haitatubu' wala kuiomba radhi Algeria kutokana na jinai zilizofanywa na Wafaransa katika zama walipoikoloni nchi hiyo ya Kiafrika.

Ofisi ya Rais Macron ilisema jana Jumatano kuwa, katu nchi hiyo haitakiri wala kuiomba msamaha rasmi Algeria kwa jinai zilizofanywa na dola hilo wakati wa ukoloni katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hata hivyo taarifa ya Ofisi ya Macron imesema rais huyo wa Ufaransa atashiriki tu katika 'harakati za kimaonyesho' za kushajiisha uwiano na utangamano.

Mwaka uliopita, Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria alisema nusu ya wakazi wa nchi hiyo waliuawa katika jinai kubwa ya umwagaji damu iliyofanywa na Ufaransa katika kipindi cha ukoloni; na kwamba jinai hizo za wakoloni zilikuwa kinyume kabisa na utu na ubinadamu na zilikinzana pia na thamani za kiutamaduni.

Jinai za Ufaransa ilipoikoloni Algeria kwa zaidi ya karne moja 

Kadhalika wanasheria wa haki za binadamu nchini Algeria wamekuwa wakisisitiza kuwa, Paris inapaswa kulipa gharama na fidia kufuatia kukiri serikali ya Ufaransa kuwatesa na kuwaua wale wote waliokuwa wakiunga mkono mapinduzi ya Algeria.

Ufaransa iliikoloni Algeria kwa miaka 132 na hatimaye nchi hiyo mwaka 1962 ikapata uhuru baada ya miaka kadhaa ya mapambano ya ukombozi ya umwagaji damu. Raia wa Algeria karibu laki tano waliaga dunia katika mapambano ya kuikomboa nchi yao.