Feb 12, 2021 07:43 UTC
  • Wafuasi wa al Bashir wazidi kutiwa mbaroni nchini Sudan

Operesheni za kuwatia mbaroni wafuasi wa serikali iliyopinduliwa ya Omar al Bashir zinaendelea baada ya makamu wa rais huyo wa zamani wa Sudan naye kutiwa pingu.

Shirika la habari la ISNA limeripoti habari hiyio na kuongeza kuwa, jana Alkhamisi, Februari 11, 2021, Hassabu Mohamed Abdalrahman, makamu wa Omar al Bashir ametiwa mbaroni katika operesheni maalumu ya kuwatia pingu maafisa wa serikali ya al Bashir. Hatua hiyo imechukuliwa huku maandamano yakiendelea nchini Sudan kiasi kwamba watawala wa hivi sasa wamelazimika kutangaza hali ya hatari katika mikoa 7 ya nchi hiyo.

Watawala wa hivi sasa wa Sudan wanawatuhumu maafisa wa serikali ya al Bashir kuwa wanawachochea watu kufanya uharibifu katika miundombinu ya nchi hiyo, kupora na kuchoma masoko na maduka katika mikoa tofauti ya nchi hiyo. 

Jenerali Omara al Bashir, rais wa zamani wa Sudan akiwa kizimbani

 

Wakati huo huo Kamati ya Kupambana na Ufisadi  na kurejesha fedha za umma kutoka mikononi mwa maafisa wa al Bashir leo imetoa hukumu ya kutiwa mbaroni wanachama wote wa chama cha Congress ya Taifa cha al Bashir ambacho kimevunjwa. Amri hiyo imetolewa kwa ajili ya kutekelezwa katika mikoa yote ya Sudan na kuwataka maafisa husika waitekeleze kuvitendo.

Katika taarifa yake kamati hiyo imesema, kuna ushahidi wa kutosha wa harakati za wanachama wa chama cha Congress ya Taifa kilichovunjwa za kuchoma moto maeneo muhimu na kuiba mali za umma.

Hukumu hiyo kali imetolewa katika hali ambayo wanaharakati wa Sudan wanatumia mitandao ya kijamii kufanya kampoeni zao. Ikumbukwe kuwa, watawala wa hivi sasa wa Sudan ni miongoni mwa watawala wa nchi za Kiarabu waliojidhalilisha kwa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags