Mgogoro wa kisiasa unaendelea nchini Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66826-mgogoro_wa_kisiasa_unaendelea_nchini_tunisia
Moto za mzozo wa kisiasa umezidi kuwa mkubwa nchini Tunisia baada ya Waziri Mkuu kumtuhumu rais wa nchi hiyo kuwa ndiye anayeikwamisha Serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2021 00:16 UTC
  • Mgogoro wa kisiasa unaendelea nchini Tunisia

Moto za mzozo wa kisiasa umezidi kuwa mkubwa nchini Tunisia baada ya Waziri Mkuu kumtuhumu rais wa nchi hiyo kuwa ndiye anayeikwamisha Serikali.

Shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kumnukuu Waziri Mkuu wa Tunisia, Hichem Mechichi akisema kuwa, kitendo cha Rais Kais Saied cha kukataa kutekeleza majukumu yake kuhusu wizara zinazofanyiwa marekebisho ya kiwizara, kinakwamisha huduma za umma na kazi za Serikali.

Waziri Mkuu Mechichi aidha amesema ana matumani Rais Kais Saied atafanya haraka kuitikia mwito wa Serikali wa kutangaza majina ya wizara zilizopendekezwa na vile vile kwa mara nyingine amemtaka rais huyo atangaze majina ya wizara zinazoshukiwa kufanya ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Aidha kwa mara nyingine tena, waziri mkuu huyo wa Tunisia amesema hatojiuzulu na kusisitiza kuwa, bado milango ya mazungumzo iko wazi kwa ajili ya kufikia utatuzi wa matatizo yote yaliyojitokeza likiwemo suala la marekebisho ndani ya Baraza la Mawaziri.

Rais Kais Saied wa Tunisia

 

Tarehe 16 mwezi uliopita wa Januari, Waziri Mkuu wa Tunisia alitangaza habari ya kubadilishwa mawaziri 11 kati ya 25 wa serikali yake na siku 10 baadaye Bunge la nchi hiyo lilipasisha mabadiliko hayo.

Mwezi Julai 2020, Rais Kais Saied wa Tunisia alimteua Hichem Mechichi kuwa Waziri Mkuu na kumpa jukumu la kuunda Serikali.

Waziri Mkuu Mechichi naye ameamua kuunda Baraza la Mawaziri la wasomi, si la wanasisa. Serikali yake ilipata imani ya Bunge mwanzoni mwa mwezi Septemba 2020. Hata hivyo mgogoro wa kisiasa umetokea nchini humo, maandamano na migomo pia imeenea.