Hizbullah yasema itaendelea kusimama na Iran mkabala wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67094-hizbullah_yasema_itaendelea_kusimama_na_iran_mkabala_wa_marekani
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema harakati hiyo ya muqawama itaendelea kusimama bega kwa bega na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukabiliana na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2021 04:12 UTC
  • Hizbullah yasema itaendelea kusimama na Iran mkabala wa Marekani

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema harakati hiyo ya muqawama itaendelea kusimama bega kwa bega na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukabiliana na Marekani.

Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika Kongamano la Waislamu na Waarabu lililofanyika jana Jumamosi chini ya kaulimbiu inayosema: Muungano Dhidi ya Kuanzisha Uhusiano wa Kawaida na Utawala wa Kizayuni.

Amesisitiza kuwa, harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupambana na njama na mipango ghalati ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Lebanon amebainisha kuwa, "sisi ni Waislamu, na bega kwa bega pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine za Kiislamu katika eneo tutashirikiana kuzima njama za Marekani."

Wanamuqawama wa Hizbullah

Sheikh Naim Qassim ameeleza bayana kuwa, siasa za Marekani za kuwawekea vikwazo wengine hazina hatima nyingine ghairi ya kushindwa na kugonga ukuta, na kwamba kadiri mashinikizo yanavyokuwa mengi ndivyo ambavyo wanaolengwa wa mashinikizo hayo wanavyozidi kusimama kidete kwa ajili ya kutetea haki zao.

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, ni haki ya mataifa ya eneo hili la Asia Magharibi kusimama na kukiabiliana na uvamizi wa madola ajinabi tena kwa kutumia njia zozote.