Wanajeshi wa Ufaransa waua tena raia wengine kadhaa nchini Mali
Kundi moja la wanamgambo wenye silaha limesema kuwa, jeshi la Ufaransa limeua raia watano wengine katika shambulio la anga kaskazini mwa Mali.
Kundi hilo la kabila la Tuareg linalopigania kujitenga huko kaskazini mwa Mali, limesema kuwa, wanajeshi wa Ufaransa wamefanya shambulizi la anga kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuua raia watano akiwemo mtoto mdogo mmoja.
Kundi hilo limelaani vikali mauaji hayo na kutaka kufanyike uchunguzi wa kimataifa na kuwafikisha kizimbani Wafaransa waliofanya jinai hiyo.
Habari hiyo imetolewa ili kukanusha madai ya wanajeshi wa Ufaransa kwamba wameua magaidi watano katika shambulio la anga kaskazini mashariki mwa Mali.
Hii si mara ya kwanza kwa wanajeshi wa dola la kikoloni la Ufaransa la barani Ulaya, kushutumiwa kufanya mauaji ya raia nchini Mali.
Huko nyuma pia, asasi moja ya kiraia iliwashutumu wanajeshi wa Ufaransa kwa kuua raia 10 katika sherehe za harusi katikati ya Mali. Wanajeshi wa Ufaransa walishindwa kukanusha mauaji hayo.
Mwaka 2012 Ufaransa ilituma wanajeshi wake nchini Mali baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi yaliyofuatiwa na mapigano makali kaskazini mwa Mali ambayo yalipelekea eneo kubwa la maeneo hayo kujitangazia uhuru wao.
Sasa hivi kuna zaidi ya wanajeshi 5,000 wa Ufaransa katika eneo la Sahel Afrika. Eneo hilo ni ukanda unaokata katikati ya jangwa la Sahara kutokea mashariki hadi magharibi. Linajumuisha kaskazini mwa Senegal, kusini mwa Mauritania, Katikati ya Mali, kusini mwa Algeria, Niger, katikati ya Chad, kusini mwa Sudan, Kaskazini mwa Sudan Kusini na Eritrea.