Daesh yaua raia 16 wa Ethiopia nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6910-daesh_yaua_raia_16_wa_ethiopia_nchini_libya
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetoa kanda mpya ya video ya kuogofya inayoonyesha namna magaidi hao wanavyowaua kinyama raia wa Ethiopia nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2016 02:20 UTC
  • Daesh yaua raia 16 wa Ethiopia nchini Libya

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetoa kanda mpya ya video ya kuogofya inayoonyesha namna magaidi hao wanavyowaua kinyama raia wa Ethiopia nchini Libya.

Kanda hiyo ya video ya dakika 29 hivi inaonyesha namna magaidi hao wa Daesh ambao walikuwa wamefunika nyuso zao walivyowaua raia wa Ethiopia kwa kuwamininia risasi kichwani huku wakiwa wamefungwa mikono na kupigishwa magoti. Baadhi ya raia 16 wa Ethiopia waliouawa na Daesh kwa kufyatuliwa risasi walikuwa wamefungwa chini ya miti na wengine wakauawa kwenye ufuo wa bahari. Habari zinasema kuwa, raia hao wa Ethiopia waliouawa na matakfiri wa Daesh katika ardhi ya Libya ni waumini wa dini ya Kikristo. Kabla ya kutekeleza ukatili huo, mmoja wa magaidi hao alisoma ujumbe unaosema: "Hawa ni wafuasi wa msalaba kutoka Kanisa la maadui huko Ethiopia, ambao wamekataa kulipa kodi ya kidini au kusilimu."

Hii sio mara ya kwanza kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kutekeleza unyama wa aina hii dhidi ya raia wa Ethiopia nchini Libya.

Mwezi uliopita wa Aprili, magaidi hao wenye misimamo ya kufurutu ada walitoa kanda nyingine ya video iliyoonyesha wakiua raia 30 wa Ethiopia wafuasi wa dini ya Kikristo kwa misingi hiyo hiyo eti ya kukataa kulipa kodi au kujiunga eti na Uislamu. Baadhi yao waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na wengine kwa kukatwa vichwa.