'Vikwazo vitaongeza ugumu katika mgogoro wa Mali, wananchi watazidi kuumia'
Siku moja baada ya Ufaransa kukata uhusiano wake wa kijeshi na nchi ya Mali, Waziri Mkuu mtarajiwa wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika amesema kuwa, nchi yake inaheshimu sheria za kimataifa lakini vikwazo vitazidisha utata katika mgogoro wa nchi hiyo na vitazidi kuwaumiza wananchi wa kawaida.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Ufaransa imetuma wanajeshi wake kuzisaidia nchi za Mali, Chad, Mauritania, Niger na Burkina Faso kupambana na wanamgambo katika eneo la Sahel Afrika.
Hata hivyo baada ya kutokea mapinduzi mengine ya kijeshi ya tarehe 24 mwezi uliopita wa Mei huko nchini Mali, Paris imeamua kukatisha ushirikiano wake wa kijeshi na Bamako ikidai kuwa itaendelea kushirikiana na serikali ya kiraia ya Mali iwapo wanajeshi waliofanya mapinduzi watairejesha madarakani serikali hiyo.
Choguel Kokalla Maïga, waziri mkuu mtarajiwa wa Mali katika serikali ya mpito, amesema siku moja baada ya Ufaransa kutangaza kukatisha ushirikiano wake wa kijeshi na Mali, kwamba Bamako inaheshimu sheria za kimataifa.
Maiga anatarajiwa kuapishwa kuwa waziri mkuu mpya wa Mali katika sherehe zitakazofanyika keshokutwa Jumatatu na kuhudhuriwa na Kanali Assimi Goita, aliyeongoza mara mbili mapinduzi ya kijeshi yakiwemo haya ya karibuni kabisa ya tarehe 24 mwezi uliopita wa Mei.
Siku hiyo hiyo ya Jumatatu inatarajiwa kwamba Mahakama ya Katiba ya Mali itamteua rasmi Kanali Assimi Goita kuwa rais wa serikali ya mpito ya Mali.
Jana Ijumaa pia, Benki ya Dunia ilisimamisha shughuli zake za kifedha nchini Mali na kusema kuwa inafuatilia kwa karibu matukio na hatua zinazochukuliwa huko nchini Mali.