Mangoush: Libya haitaruhusu ardhi yake itumiwe dhidi ya nchi nyingine
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71160-mangoush_libya_haitaruhusu_ardhi_yake_itumiwe_dhidi_ya_nchi_nyingine
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya amesema kuwa nchi yake haitakubali kutumiwa kama kituo cha kuvuruga amani na utulivu katika kanda hiyo ya Afrika au kutumiwa ardhi na anga yake dhidi ya upande wowote mwingine.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 12, 2021 02:51 UTC
  • Mangoush: Libya haitaruhusu ardhi yake itumiwe dhidi ya nchi nyingine

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya amesema kuwa nchi yake haitakubali kutumiwa kama kituo cha kuvuruga amani na utulivu katika kanda hiyo ya Afrika au kutumiwa ardhi na anga yake dhidi ya upande wowote mwingine.

Najla Mangoush ameyasema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari mjini Tripoli akiwa pamoja na Waziri wa Serikali katika Mambo ya Nje wa Uingereza, James Cleverly.

Mangoush amezishukuru nchi zote zinazoisadia Tripoli kuchukua maamuzi ya kujitegemea ya kisiasa ili kuzishinikiza nchi za kigeni kuacha kuingilia mambo ya ndani ya Libya. 

Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya yametolewa baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzitaka nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, kuharakisha kuondoa mamluki wao katika ardhi ya Libya, suala ambalo halijatekelezwa hadi hivi sasa licha ya mapatano ya kusitisha vita yaliyosainiwa na makundi hasimu ya Libya Oktoba 23 mwaka jana. Makubaliano hayo yanasisitiza udharura wa mamluki hao kuwa wameondoka katika ardhi ya Libya katika kipindi cha siku 90 tangu baada ya kutekelezwa kwake. 

Mapema mwezi huu pia Spika wa Bunge la Libya alisema majeshi ya nchi za nje na askari mamluki wa kigeni wanapaswa kuondoka katika ardhi ya Libya.

Aguila Saleh Issa alisema kuwa Libya inasumbuliwa na migawanyiko, na ametoa wito wa kuondoka majeshi na mamluki wa kigeni nchini humo na kuangamizwa makundi ya waasi. 

Majeshi yote ya nchi za kigeni yanapaswa kuondoka katika ardhi ya Libya kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo ambao umepangwa kufanyika tarehe 24 Disemba mwaka huu wa 2021.