Mahakama Tunisia yaagiza kuachiwa huru kiongozi wa upinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71324-mahakama_tunisia_yaagiza_kuachiwa_huru_kiongozi_wa_upinzani
Vyombo vya mahakama nchini Tunisia vimeagiza kuachiwa huru kiongozi wa upinzani, Nabil Karoui, miezi sita baada ya kutiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na kukwepa kodi. 
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2021 03:37 UTC
  • Mahakama Tunisia yaagiza kuachiwa huru kiongozi wa upinzani

Vyombo vya mahakama nchini Tunisia vimeagiza kuachiwa huru kiongozi wa upinzani, Nabil Karoui, miezi sita baada ya kutiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na kukwepa kodi. 

Karoui amekuwa katika mgomo wa kula chakula tangu tarehe 5 mwezi huu akilalamikia kushikiliwa kwa muda mrefu. 

Mahakama nchini Tunisia imeonekana kuzingatia kwamba, Nabil Karoui mwenye umri wa miaka 57 ambaye ni kiongozi wa chama cha Qalb Tounes, amekuwa korokoroni kwa muda mrefu ikilinganishwa na muda unaoruhusiwa kisheria. Hayo yameelezwa na wakili wa kiongozi huyo wa upinzani, Nazih Souii.

Karoui ambaye ni mwasisi wa televisheni binafsi ya Nessma huko Tunisia ambayo kwa upande mmoja inamilikiwa na waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi amekuwa akikabiliwa na mashktaka tangu mwaka 2017 kwa tuhuma za kutakatisha pesa na kukwepa kodi. Nabil Karoui alikamatwa mwaka 2019  wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais nchini Tunisia.