May 16, 2016 16:06 UTC
  • Jeshi la Nigeria: Kundi la Boko Haram limepata pigo kubwa

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limepata mafanikio makubwa katika operesheni yake ya pamoja na jeshi la Cameroon dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Taarifa ya jeshi la Nigeria imeeleza kuwa, operesheni ya pamoja ya jeshi hilo na wenzao wa Cameroon imetoa pigo kubwa kwa wanamgambo wa Boko Haram.

"Operesheni hiyo ya pamoja ya jeshi la Nigeria na Cameroon imeangamiza vituo vitatu vya mafunzo vya Boko Haram nchini Nigeria," imesema taarifa ya jeshi la Nigeria.

Aidha imeripotiwa kwamba, makumi ya wanamgambo wa Boko Haram wameuawa huku watu 50 waliokuwa wakishikiliwa mateka na wanamgambo hao wakikombolewa.

Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeshaua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kuyakimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Mbali na Nigeria wanamgambo hao sasa wanafanya vitendo vya kigaidi katika nchi jirani za Chad, Niger, Cameroon na hata Benin.

Serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria inaendelea kuandamwa na tuhuma za kushindwa kulitokomeza kundi hilo la kigaidi ambalo limekuwa tishio kubwa kwa usalama wa nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika.

Tags