Daesh waua makumi ya raia wa Libya kwa tuhuma za kufanya mazingaombwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7324-daesh_waua_makumi_ya_raia_wa_libya_kwa_tuhuma_za_kufanya_mazingaombwe
Shirika la kutetea haki za binaadamu limetangaza habari ya kuuawa makumi ya watu na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh katika miji ya Sirte na Misrata, kaskazini mwa Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 18, 2016 22:20 UTC
  •  Daesh waua makumi ya raia wa Libya kwa tuhuma za kufanya mazingaombwe

Shirika la kutetea haki za binaadamu limetangaza habari ya kuuawa makumi ya watu na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh katika miji ya Sirte na Misrata, kaskazini mwa Libya.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo mapema leo imesema kuwa, kwa akali watu 49 wameuawa na wanachama wa kundi la Daesh katika mji wa Sirte, huku makumi ya wengine wakiuawa katika mji wa Misrata wa nchi hiyo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wahanga hao waliuawa kwa kukatwa shingo zao na wengine kwa kupigwa risasi. Kadhalika shirika la kutetea haki za binaadamu limefafanua kuwa, kundi hilo la kigaidi limekuwa likiwaua mateka na wapinzani wake wa kisiasa kwa tuhuma bandia ikiwemo kufanya ujasusi, kujihusisha na vitendo vya uchawi ama kufanya mazingaombwe. Kufuatia hali hiyo, shirika hilo limelitaka Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi kuhusiana na jinai hizo nchini Libya. Kadhalika shirika hilo limelitaka baraza hilo kuwapandisha kwenye vyombo vya sheria wanachama wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri la Daesh na wanachama wa makundi mengine yenye misimamo ya kufurutu ada ndani ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.