Khalifa Haftar: Ulaya haiupi uzito utulivu na usalama nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7333-khalifa_haftar_ulaya_haiupi_uzito_utulivu_na_usalama_nchini_libya
Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Libya amesema, ana wasiwasi na siasa za nchi za Ulaya kuhusiana na Libya na inaonekana kuwa nchi hizo hazilipi uzito suala la usalama wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 18, 2016 22:21 UTC
  • Khalifa Haftar: Ulaya haiupi uzito utulivu na usalama nchini Libya

Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Libya amesema, ana wasiwasi na siasa za nchi za Ulaya kuhusiana na Libya na inaonekana kuwa nchi hizo hazilipi uzito suala la usalama wa nchi hiyo.

Shirika la habari la ISNA limemnukuu Khalifa Haftar, mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Libya akisema jana (Jumatano) katika mahojiano na kanali ya televisheni ya "Libya al Hadath" kwamba, ana wasiwasi na misimamo ya madola makubwa duniani kuhusiana na suala la kupambanana ugaidi. Amesema licha ya kwamba jeshi la Libya limewekewa vikwazo vya silaha, lakini linaiwakilisha dunia nzima katika kupambana na ugaidi. Amesema, kama nchi za dunia hazitalisaidia jeshi la Libya, basi ugaidi utaenea katika nchi nyingine za duniani hususan za barani Ulaya. Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Libya ameongeza kuwa, njia pekee ya kuitoa Libya kwenye mgogoro wake wa hivi sasa ni kuangamizwa maeneo wanayokusanyika magaidi kaskazini mwa nchi hiyo. Amesisitiza kuwa, kama dunia itafikia mwafaka kuhusu kuondolewa vikwazo vya silaha jeshi la Libya, basi bila ya shaka yoyote magenge hayo ya kigaidi yataangamizwa nchini humo. Kundi la kigaidi la Daesh limetumia vibaya ukosefu wa utulivu wa kisiasa, kujipenyeza katika mji wa Sirte wa kaskazini mwa Libya ulioko umbali wa kama kilomita 100 tu kutoka fukwe za barani Ulaya na kila leo linafanya mashambulizi zaidi katika maeneo mengine ya Libya.