Aug 10, 2021 07:40 UTC
  • Watu zaidi ya 51 wauawa katika hujuma ya magaidi nchini Mali

Zaidi ya watu 51 wameuawa katika hujuma iliyofanyika kaskazini mwa Mali karibu na mpaka wa nchi hiyo na Niger.

Magaidi wanatuhumiwa kuwa walihusika na mashambulizi hayo ingawa hakuna kundi lololote lililodai kuhusika.

Mashambulio hayo yalifanyika Jumapili katika maeneo kadhaa ya Karou, Ouatagouna, Dirga na Déoutéguef. Maeneo yote haya yako kwenye barabara inayoelekea Kaskazini hadi kwenye mpaka wa Niger. 

Miongoni mwa waliouawa au kujeruhiwa watoto ndio wengi zaidi ambapo walioshuhudia wanasema washambuliaji walikuwa wakifyatulia risasi 'chochote kilichokuwa hai'.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali

Hayo yanajiri wakati ambao mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alilitaka Baraza la Usalama la Umoja huo kukitia nguvu na kukiimarisha kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Mali, kwa kifupi MINUSMA ili kukabiliana na mashambulizi yanayozidi kuongezeka ya magenge ya kigaidi na ukufurishaji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelishauri Baraza la Usalama liidhinishe kuongezwa idadi ya wanajeshi na askari wa MINUSMA hadi 17,278, idadi ambayo itakuwa kubwa zaidi kuwahi kutumwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kulinda amani huko Mali. Kikosi cha kulinda amani nchini Mali, MINUSMA  kiliundwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2013.

 

Tags