Ujerumani yafungua tena ubalozi wake huko Tripoli, Libya
Ujerumani imefungua tena ubalozi wake huko Libya baada ya kufungwa kwa miaka minane.
Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani jana Alhamisi alishiriki katika hafla ya kufunguliwa tena ubalozi wa nchi hiyo huko Tripoli mji mkuu wa Libya.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Maas amesema: "Leo tunataka kuonyesha kufunguliwa tena ubalozi wa Ujerumani na kwamba Berlin itaendelea kuwa mshirika wa kutumainiwa wa Libya."
Balozi wa Ujerumani aliondoka Libya mwaka 2014 kutokana na ukosefu wa amani na hali ya mchafukoge nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amepongeza juhudi za Libya za kurejesha amani nchini humo.
Heiko Maas aidha ameashiria hatua zilizopigwa huko Libya na kusema, kufanyika uchaguzi na kuondoka wanajeshi wa nchi ajinabi nchini Libya ni hatua muhimu, na kwa sababu hiyo maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao cha Berlin kuhusu Libya yanapasa kutekelezwa.
Amesema leo hii Libya ina serikali ya umoja wa kitaifa, mzingiro wa mafuta umeondolewa na ubebaji silaha umepungua kwa kiasi kikubwa.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.