Algeria na Libya zakubaliana kufunguliwa tena ubalozi wa Algeria huko Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i74774-algeria_na_libya_zakubaliana_kufunguliwa_tena_ubalozi_wa_algeria_huko_tripoli
Rais wa Algeria na Naibu Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya wamekubaliana kufungua tena ubalozi wa Algeria huko Tripoli mji mkuu wa Libya.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 17, 2021 22:01 UTC
  • Algeria na Libya zakubaliana kufunguliwa tena ubalozi wa Algeria huko Tripoli

Rais wa Algeria na Naibu Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya wamekubaliana kufungua tena ubalozi wa Algeria huko Tripoli mji mkuu wa Libya.

Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria amemlaki Makamu Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya Musa al Koni katika ziara rasmi mjini Algiers katika fremu ya mashauriano yanayoendelea kati ya nchi mbili hizo jirani.

Musa al Koni Makamu Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Abdelmajid Tebboune kuhusu suala la kufungua tena ubalozi wa Algeria mjini Tripoli. Viongozi hao wawili wamesisitiza ulazima wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya na kuitisha chaguzi za Rais na Bunge katika muda uliopangwa bila ya kuingiliwa na nchi ajinabi. 

Rais Tebboune amesisitiza msimamo wa Algeria kwamba inaunga mkono suala la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya kwa kuanzisha taasisi za serikali na kupinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Libya. 

Kwa upande wake, Musa al Koni Makamu Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya ameshukuru jitihada endelevu za Algeria kwa maslahi ya nchi mbili hizo rafiki.

Moussa al Koni, Makamu Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya

Vilevile amepongeza uamuzi wa Algeria wa kufungua tena ubalozi wake mjini Tripoli, ubalozi mdogo huko Sabha, safari za ndege kutoka Algiers hadi Tripoli na kufungua vivuko vya mpakani vya Ghat na Ghadames.