Libya yapinga kusimamishwa kazi Waziri wa Mambo ya Nje kabla ya uchaguzi
Serikali ya Libya imepinga uamuzi wa Baraza la Rais la nchi hiyo wa kumsimamisha kazi Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, wiki chache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Katika taarifa yake jana Jumapili, Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) imesema Baraza la Rais la nchi hiyo halina mamlaka ya kisheria ya kumsimamisha kazi Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Najla al-Mangoush.
Taarifa hiyo imempongeza mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Libya kwa jitihada zake za kujaribu kuipatia ufumbuzi mizozo ya kisiasa iliyopo, kelekea uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imesema jukumu la kuteua, kusimamisha, kuchunguza na hata kuwafuta kazi maafisa wa serikali ni la Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Siku ya Jumamosi, Baraza la Rais la nchi hiyo liltangaza kumsimamisha kazi Najla Mangoush, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na kumzuia kusafiri nje ya nchi, likimtuhumu kuwa halihusishi baraza hilo katika maamuzi muhimu yanayohusu sera za nje za nchi hiyo.
Uamuzi wa kumsimamisha kazi al-Mangoush umekuja siku chache kabla ya kufanyika Kongamano la Kimataifa la Paris, la kushinikiza kufanyika uchaguzi mkuu nchini Libya kama ilivyopangwa. Uchaguzi huo wa Libya umeratibiwa kufanyika tarehe 24 mwezi ujao wa Disemba.