Familia ya mwanamke wa Kenya aliyeuawa yalishtaki jeshi la Uingereza
Familia ya mwanamke wa Kenya anayedaiwa kuuawa na askari wa Uingereza imelishtaki jeshi la UK ikitaka lishurutishwe kutoa majibu ya kitendawili cha mauaji hayo.
Hayo yamefichuliwa leo Jumatano na Tessa Gregory, wakili katika Shirika la Mawakili la Leigh Day linalofuatilia faili la mauaji ya mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 21 wakati akiuawa mwaka 2012.
Mwansheria huyo amesema familia ya Agnes Wanjiru imewataka waifunguliwe mashitaka Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, kwa kuficha au kufeli kuchunguza mauaji hayo yaliyofanywa na mwajeshi wa nchi hiyo ya Ulaya katika ardhi ya Kenya.
Gregory amesema mteja wao anataka haki kwa Agnes Wanjiru, na vile vile majibu kwa masuali mazito yanayoyazunguka mauaji hayo, kama vile iwapo jeshi la Ulaya lilifahamu chochote kuhusu mauaji hayo, na pia kwa nini Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo haichukua hatua yoyote juu ya ukatili huo katika kipindi cha miaka 9 iliyopita.
Mwezi uliopita, gazeti la Uingereza la Sunday Times liliripoti kuwa, askari mmoja wa UK amekiri kuhusika na mauaji ya mwanamke huyo wa Kenya, na akaeleza kuwa aliwafahamisha wanajeshi wenzake juu ya ukatili huo, sambamba kuwaonesha sehemu alikoficha mwili wa marehemu.
Mwili wa Agnes Wanjiru ulipatikana katika pipa la maji mnamo mwaka 2012 mjini Nanyuki katikati mwa Kenya, nyuma ya hoteli moja inayopakana na kambi ya kudumu ya jeshi la Uingereza. Polisi ya Kenya wiki iliyopita ilisema itafungua upya faili la mauaji ya mama huyo aliyekuwa na mtoto mmoja.