Wafuasi wa upinzani DRC kuandaa maandamano Kinshasa leo
Vyombo vya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimeupa idhini muungano wa vyama vya upinzani nchini humo kuandaa maandamano katika mji mkuu Kinshasa hii leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani katika mkoa wa Kinshasa, Emmanuel Akweti ametangaza katika mkutano na wajumbe wa muungano wa upinzani kuwa, Mkuu wa mji wa Kinshasa hajapinga kufanyika maandamano ya muungano wa vyama vya upinzani mjini hapo leo Alhamisi, licha ya Julien Paluku, Gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini, kupiga marufuku maandamano ya wapinzani wa serikali katika mkoa huo. Aidha serikali ya DRC imepiga marufuku maandamano ya wapinzani katika miji ya Lubumbashi na Mbuji Mayi. Upinzani umeitisha maandamano hayo kwa lengo la kulalamikia hukumu iliyotolewa na mahakama ya katiba ya nchi hiyo tarehe 11 mwezi huu ya kutaka kuendelea kusalia madarakani Rais Joseph Kabila kinyume na sheria.
Hivi karibuni, Maman Sidikou, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alielezea wasiwasi wa umoja huo kufuatia kuongezeka mizozo ya kisiasa nchini humo na kusisitiza kuwa, mikwaruzano hiyo ya kisiasa inaweza kuharibu zaidi hali ya mambo nchini humo na kukwamisha mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta njia za kufanyika uchaguzi mkuu kwa ufanisi.
Hivi karibuni muungano wa vyama kadhaa vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulimtangaza Moise Katumbi, mwanasiasa anayeonekana kuwa tishio kwa Rais Jioseph Kabila, kuwa mgombea wake katika uchaguzi ujao wa Rais unaotazamiwa kufanyika Novemba mwaka huu.