Umoja wa Mataifa: Hakuna ramani mpya ya njia kwa ajili ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78268-umoja_wa_mataifa_hakuna_ramani_mpya_ya_njia_kwa_ajili_ya_libya
Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNMSIL) amesema hakuna ramani mpya ya njia kwa ajili ya Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 21, 2021 02:38 UTC
  • Jean Alam
    Jean Alam

Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNMSIL) amesema hakuna ramani mpya ya njia kwa ajili ya Libya.

Kwa mujibu wa gazeti la Al-Quds Al-Arabi, Jean Alam abaye alikuwa akizungumzia uvumi wa kuwepo ramani mpya ya njia kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Libya amesema, taarifa zinazohusishwa na "Stephanie Williams", Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika mitandao ya kijamii juu ya kuwepo ramani mpya njia kwa ajili ya uchaguzi wa Libya, hazina ukweli.

Jean Alam amesema: "Habari hizi ni za upotoshaji na si sahihi, na zimechapishwa katika mfumo wa habari za uongo kwa lengo la kuzuia juhudi za upatanishi na kupotosha maoni ya umma."

Alam pia amesema Williams bado yuko katika harakati za kushauriana na kusikiliza maoni ya makundi mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiusalama ya Libya.

Wakati huo huo Emad al-Sayeh, Mkuu wa Tume Kuu ya Taifa ya Uchaguzi. ya Libya amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba: "Tangazo la kuahirishwa uchaguzi haliko chini ya mamlaka ya tume hiyo na kwamba Bunge lililotoa amri ya kufanyika uchaguzi ndilo lenye mamlaka ya kutoa amri ya kusimamishwa zoezi hilo."

Mapema mwezi huu Baraza Kuu la serikali ya Libya lilipendekeza kuwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ufanyike mwezi Februari mwakani sawa na ule wa Bunge badala ya tarehe 24 Disemba mwaka huu.

Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi Libya, Omar Abdel Aziz Bushah alisema mchakato wa sasa wa uchaguzi unaweza kuchelewesha kutokana na masuala mbalimbali yanayoitatiza Tume Kuu ya Taifa ya Uchaguzi.