Tume ya uchaguzi Libya: Uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 24 Januari
Tume Kuu ya Taifa ya Uchaguzi nchini Libya (HNEC) imetangaza kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliokuwa umeakhirishwa, utafanyika tarehe 24 ya mwezi huu wa Januari.
Mwenyekiti wa tume hiyo Emad Al-Sayeh amesema, tarehe hiyo imepitishwa kwa kufuata muda wa kisheria wa siku 30 tokea tarehe ulipoakhirishwa uchaguzi huo.
Aidha, Al-Sayeh amesisitiza kuwa, tume ya uchaguzi itahakikisha inatoa orodha ya wagombea bila kusitasita wala kuzusha utata wowote.
Uchaguzi mkuu wa Libya ulipangwa kufanyika tarehe 24 Desemba, lakini ukaakhirishwa kutokana tofauti zilizojitokeza kuhusu sheria ya uchaguzi ikiwemo sifa za wagombea na nafasi ya Idara ya Mahakama katika kuchunguza malalamiko ya uchaguzi.
Jumatatu ya wiki iliyopita bunge lilipendekeza uchaguzi wa rais ufanyike katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kutoa fursa ya kufanyika mazungumzo mapana baina pande mbalimbali.
Kabla ya hapo, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams alisema, jambo la kufikiriwa zaidi baada ya kuakhirishwa uchaguzi wa rais liwe ni juu ya namna uchaguzi wenyewe utakavyofanyika, si juu ya hatima ya serikali ya muda.
Baada ya mahakama ya rufaa ya Tripoli kubatilisha uamuzi wa kumzuia Saiful-Islam Gaddafi na Khalifa Haftar kugombea urais wa Libya, serikali ya muda ya nchi hiyo imekabiliwa na changamoto za tofauti zilizozuka kuhusu tarehe ya kufanyika uchaguzi kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, hofu ya juu ya ushawishi wa madola ya kigeni katika uchaguzi huo.../