Ufaransa kuondoka Mali, yasema itasalia katika eneo la Sahel Afrika
-
Jean-Yves Le Drian
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian ametangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wataendelea kupambana na kile alichokitaja kuwa 'ugaidi' katika eneo la Sahel na si nchini Mali.
Le Drian amesema, wanajeshi wa Ufaransa watajiimarisha katika eneo la Sahel barani Afrika na si nchini Mali. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alieleza hayo jana baada ya kikao chake na mawaziri wenzake wa Ulaya kwa njia ya mtandao.
Katika kikao hicho, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ulaya na mwenzao wa Ufaransa walijadili hatima ya nchi zao wakati huu ambapo makundi ya wanamgambo wenye silaha magharibi mwa Afrika wamezidisha mashambulizi katika eneo hilo.
Hitilafu zimeongezeka kati ya Ufaransa na Mali ambapo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kuwa kuna haja ya kufanyika marekebisho kuhusu uwepo wa wanajeshi wa nchi yake huko Mali.
Wanajeshi wa Ufaransa katika eneo la Sahel barani Afrika wanahudumu katika oparesheni Barkhane na ni sehemu ya kikosi kazi cha kimataifa cha Takuba. Viongozi wa Sahel na Ufaransa kesho watakutana kujadili stratejia mpya. Kinyume na mkutano wao wa mwaka 2020, ni Marais 3 kati ya 5 wa eneo la Sahel ndio watakaoshiriki mkutano huo. Marais wa Chad, Nigeria na Mauritania ndio wakaohudhuria mkutano huo.
mapema mwezi huu Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maiga, aliishutumu serikali ya kikoloni ya Ufaransa kwa vitendo vyake dhidi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na kusema kuwa, Wafaransa walipaswa kuisaidia Mali, lakini badala yake wanayasaidia magenge ya kigaidi yanayopigania kujitenga na wanazichochea nchi za Ulaya ziliwekee vikwazo taifa hilo la Kiafrika.
Maiga alisema: Ufaransa haiheshimuu makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na badala yake mkoloni huyo kizee wa Ulaya anayasaidia makundi ya kigaidi na kuigawa vipande vipande nchi ya Mali.
Serikali ya Mali pia imemtimua balozi wa Ufaransa nchini humo kutokana na matamshi yaliyoja uhasama na matusi ya viongozi wa Ufaransa dhidi ya serikali ya Bamako.