Kuendelea mgogoro Tunisia kwa kuvunjika mazungumzo ya serikali na wapinzani
Mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia umechukua sura na muelekeo mpana zaidi baada ya kuvunjika mazungumzo baina ya serikali na muungano wa asasi za ajira, ambao ndio mwamvuli mkubwa zaidi wa miungano mbalimbali inayopinga sera za serikali ya sasa ya nchi hiyo; na sasa muungano huo umewatolea mwito wananchi kushiriki kwenye mgomo wa umma wa nchi nzima.
Ofisi ya utendaji ya muungano wa asasi za ajira imetoa taarifa ikiwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mgomo huo ili kuhakikisha unapata mafanikio yaliyokusudiwa.
Tunisia ilitumbukia kwenye dimbwi la mgogoro mkubwa wa kisiasa ulioanza tarehe 25 Julai 2021, wakati rais Kais Saeid alipotangaza uchukuaji wa hatua kadhaa kubwa na zisizo za kawaida ikiwemo kufuta mamlaka na kusimamisha shughuli za bunge, kumuuzulu spika na waziri mkuu na kuivunja serikali yake, kuitisha kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba, kuwaondolea kinga wabunge na kulivunja jopo la usimamizi wa katiba; na hivyo kusababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa katika nchi hiyo. Hatua hizo za rais Saeid zimekabiliwa na wimbi kubwa la upinzani na malalamiko ya vyama na mirengo mikuu ya kisiasa ya Tunisia.

Kama vile haitoshi, hivi karibuni, Rais Kais Saeid aliwaachisha kazi pia majaji 57 kwa tuhuma za ufisadi, hatua ambayo imeshadidisha hali mbaya iliyopo ya mgogoro huo wa kisiasa na kufuatiwa na mgomo ulioshirikisha majaji wengi wa nchi hiyo.
Vuguvugu la Khalas limesema, hatua ya Kais Saeid ya kuwauzulu majaji inapingana na msingi wa kutenganisha kazi za mihimili ya dola na kubainsha kuwa uingiliaji wa kutisha unaofanywa na rais katika utendaji wa idara ya mahakama unatumika kama wenzo wa kufanyia dhulma na uonevu na njia ya kuielekeza nchi kwenye makabiliano kati ya serikali, vyama vya siasa na miungano ya asasi mbalimbali.
Mbali na hatua nyingine kadhaa alizochukua, rais wa Tunisia ameng'ang'ania pia msimamo wake wa kuitisha kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Julai 25, jambo ambalo limevikasirisha sana vyama vya siasa na raia wa kawaida wa nchi hiyo. Kwa mtazamo wao, mabadiliko ya katiba yaliyokusudiwa kufanywa yanalenga kuimarisha madaraka ya rais na kumwongezea mamlaka; na yanakinzana na matarajio waliyokuwa nayo awali Watunisia. Kwa mtazamo wa wapinzani wa Kais Saeid, hatua za kiongozi huyo ni sawa na mapinduzi dhidi ya matunda ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia vuguvugu la mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali. Kwa sababu hiyo, harakati iitwayo "Kampeni ya kitaifa ya kukabiliana na kura ya maoni Tunisia" imetoa mwito wa kususiwa kura hiyo ya maoni na ikaeleza yafuatayo katika taarifa yake: "Sisi hatukubali kurudi tena kwenye awamu ya udikteta; na hatua za Kais Saeid ni mapinduzi dhidi ya mafanikio ya kidemokrasia; na lengo lake ni kuimarisha utawala unaopiga vita uhuru".

Katika upande mwingine, kuendelea mgogoro nchini Tunisia kumepelekea kuongezeka harakati za kisiasa na juhudi za kuutatua mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo. Jitihada za karibuni zaidi zimefanywa na muungano wa asasi za ajira, kwa kufanya mazungumzo na serikali juu ya utekelezaji wa mageuzi na malalamiko ya muungano huo dhidi ya hatua ya kusimamishwa mishahara.
Kabla ya kufanyika mazungumzo hayo, Nouruddin at-T'abubi, Katibu Mkuu wa muungano wa asasi za ajira Tunisia aliihutubia hadhara kubwa ya wafanyakazi wa vibarua akisisitiza kuwa, wanapinga ubabaishaji unaofanywa kuhusiana na mikataba yenye madhara na isiyo ya haki.
Hata hivyo mazungumzo ya serikali na muungano wa asasi za ajira yamevunjika kwa kutopatikana tija iliyokusudiwa; na hivi sasa muungano huo umeitisha mgomo wa nchi nzima ulioanza jana Jumatano. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, mgomo huo utafikisha ujumbe utakaodhihirisha nafasi yake na kiwango cha taathira iliyonayo ndani ya Tunisia.

Muungano wa asasi za ajira umesisitiza kwa kusema: ukurasa wa mazungumzo umeshafungwa moja kwa moja. Maana ya msimamo huu ni kukata mawasiliano na rais na kukata mawasiliano na njia anayofuata.
Kutokana na hali iliyojitokeza, hakuna matumaini kuwa tofauti zilizopo katika mgogoro wa Tunisia zitaweza kutatuliwa kwa njia ya amani. Vyama vya siasa vimetangaza kwamba vitaendeleza maandamano na kuisusia kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba huku Rais Kais Saeid akisisitiza kutekeleza sera zake bila kujali malalamiko na upinzani uliopo dhidi yake. Hii ni sawa na kusema kuwa, siku za mgogoro mkubwa zaidi zinainyemelea nchi hiyo.../