Kuendelea maandamano ya Watunisia wanaopinga kura ya maoni ya katiba
Mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia umeshtadi na kupamba moto zaidi. Sambamba na kukaribia tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba, maelfu ya Watunisia wameendeleza maandamano ya kupinga kura hiyo ya maoni.
Kwa miezi kadhaa sasa hali ya kisiasa imechafuka na kuvurugika nchini Tunisia. Chanzo cha yote ni hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Kais Saeid ikiwemo kusimamisha shughuli za bunge, kumuuzulu spika na waziri mkuu na kuitisha kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba. Saeid amewaondolea kinga pia wabunge pamoja na kulivunja jopo la usimamizi wa katiba.
Rais wa Tunisia amechukua hatua pia ya kuwauzulu majaji 57 aliowatuhumu kuhusika na ufisadi wa fedha na kuunga mkono ugaidi kupitia kile alichodai kuwa mkakati wa kuusafisha mhimili wa idara ya mahakama. Hatua zote hizo za Kais Saeid zimechukuliwa huku zikipingwa vikali na wananchi pamoja na vyama vya siasa, ambao wanasisitiza kuwa zinakwenda kinyume na matarajio ya umma na matunda yaliyopatikana katika vuguvugu la mapinduzi ya mwaka 2011 ambayo ni kurasimisha demokrasia katika nchi hiyo.
Licha ya maandamano na malalamiko yote hayo, Rais wa Tunisia angali ameng'ang'ania msimamo wake wa kuitisha kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba. Kwa mujibu wa rasimu ya katiba mpya, madaraka ya rais yataongezwa na yeye ndiye atakayekuwa pia na mamlaka ya kumteua waziri mkuu. Kifungu cha katiba ya sasa kinachoutambua Uislamu kuwa ndio dini rasmi ya Tunisia, nacho pia kimefutwa katika rasimu hiyo.
As-Sadiq Bal'iid, mratibu wa kamati ya taifa ya mashauriano ya utungaji katiba mpya ya Tunisia ameizungumzia nukta hiyo kwa kusema: "katika katiba mpya, rais wa Tunisia ndiye atakayemteua waziri mkuu; na serikali itageuzwa kuwa taasisi ya utawala ya kuleta ubunifu na jukumu lake halitakuwa la utendaji. Katika katiba mpya, rais atakuwa pia na mamlaka zaidi."
Kwa mtazamo wa wapinzani wa Kais Saeid, hatua za kiongozi huyo ni sawa na mapinduzi dhidi ya matunda ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia vuguvugu la mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali. Kwa sababu hiyo, harakati iitwayo "Kampeni ya kitaifa ya kukabiliana na kura ya maoni Tunisia" imetoa mwito wa kususiwa kura hiyo ya maoni na ikaeleza yafuatayo katika taarifa yake: "Sisi hatukubali kurudi tena kwenye awamu ya udikteta; na hatua za Kais Saeid ni mapinduzi dhidi ya mafanikio ya kidemokrasia; na lengo lake ni kuimarisha utawala unaopiga vita uhuru".
Wapinzani wa rais Saeid wanaitakidi kuwa katiba mpya iliyopendekezwa inampa rais mamlaka makubwa katika nyuga za siasa na uchumi ya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Kwa sababu hiyo, An-Nahdhah, ambacho ni moja ya vyama vikubwa zaidi ya vya siasa nchini Tunisia kimesisitiza kuwa kitaisusia kura hiyo ya maoni ya katiba. "Kampeni ya kitaifa ya kukabiliana na kura ya maoni Tunisia" nayo pia imetoa tangazo ikisema: "tunataka watu wasusie na wasishiriki katika kura ya maoni ya Julai 25".
Hayo yanajiri na licha ya upinzani mkubwa wa vyama na mirengo ya kisiasa, rais Saeid ameshikilia msimamo wake wa kukamilisha zoezi la kura ya maoni huku akiwatolea mwito wananchi kujitokeza kwa wingi na kuunga mkono mabadiliko ya katiba.
Mgogoro wa kisiasa wa Tunisia umeshtadi wakati uchumi wa nchi hiyo unapita katika kipindi kigumu. Na kutokana na hali hiyo, siku chache zilizopita wafanyakazi wa sekta ya umma walishiriki katika mgomo mkubwa, kuitikia mwito uliotolewa na chama kikuu cha wafanyakazi nchini Tunisia. Mgomo huo ni wa kulalamikia uamuzi wa serikali wa kukataa kuongeza mishahara, na uwezo duni wa kumudu gharama za maisha kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kifedha. Ukweli ni kwamba, hali mbaya ya uchumi ambayo haijawahi kushuhudiwa Tunisia tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake mwaka 1956 kutoka kwa mkoloni Ufaransa, inadhihirisha kufeli na kugonga mwamba hatua za uvukaji mipaka ya sheria zilizochukuliwa na Kais Saeid.
Aabir Musa, kiongozi wa chama cha katiba huru anasema: "wanachi wana njaa na uwezo wa kifedha wa kununua umepungua na uchumi wa nchi unaelekea kuporomoka, lakini Saeid hajali chochote; kitu pekee kilicho muhimu kwake yeye ni kufanikisha mipango yake binafsi."
Alaa kulli hal, inavyoonekana Tunisia itaendelea kushuhudia kipindi cha mtikisiko mkubwa wa kisiasa hadi siku ya kufanyika kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo.../