Watu wasiopungua 21 wauawa katika matukio matatu ya ufyatuaji risasi Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i85704-watu_wasiopungua_21_wauawa_katika_matukio_matatu_ya_ufyatuaji_risasi_afrika_kusini
Watu wasiopungua 21 wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika matukio matatu tofauti ya ufyatuaji risasi yaliyotokea kwenye vilabu na kumbi za starehe nchini Afrika Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2022 22:05 UTC
  • Watu wasiopungua 21 wauawa katika matukio matatu ya ufyatuaji risasi Afrika Kusini

Watu wasiopungua 21 wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika matukio matatu tofauti ya ufyatuaji risasi yaliyotokea kwenye vilabu na kumbi za starehe nchini Afrika Kusini.

Polisi wanaendelea na uchunguzi huku taarifa za awali zikionyesha kuwa hakuna mtu au watu wowote waliotiwa nguvuni kuhusiana na matukio hayo yaliyotokea Jumapili na ambayo hakuna dalili zinazoonyesha kuwepo uhusiano baina yao.

Tukio la kwanza lilitokea usiku wa manane wa kuamkia jana wakati watu wapatao watatu walipowafyatulia risasi watu waliokuwa kwenye baa moja ya mtaa wa Orlando ulioko kwenye mji wa Soweto kusini mwa Johanesburg.

Polisi imethibitisha kuwa watu 15 wameuawa katika shambulio hilo na wengine wanane wamejeruhiwa, watatu miongoni mwao wako mahututi.

Imefahamika pia kuwa watu wote waliouawa katika tukio hilo walikuwa na umri wa miaka 19 hadi 35. Manusura na mashahidi wa mauaji hayo wamesema, watu hao waliokuwa na bunduki walifyatua risasi kiholela kwenye umati uliokuwa umekusanyika kwenye baa hiyo bila sababu yoyote. 

Moja ya maeneo ulipotokea ufyatuaji risasi

Watu wengine wawili waliuawa na wanne walijeruhiwa wakati watu wenye silaha walipowafyatulia risasi watu waliokuwa kwenye baa ya Mputlane katika kitongoji cha Katlehong kusini mwa Johanesburg pia.

Tukio la tatu la ufyatuaji risasi lilitokea kwenye baa ya Sweetwaters iliyoko katika mji wa Pietermaritzburg, makao makuu ya jimbo la Kwazulu Natal, ambapo watu wanne waliuawa na wanane walijeruhiwa na kulazwa hospitali.

Matukio hayo ya ufyatuaji risasi yamejiri baada ya kupita wiki mbili tangu yalipotokea maafa ya klabu ya starehe ya eNyobeni ambapo vijana wadogo 21 walifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. 

Tukio hilo liliibua mjadala kuhusu vijana wanaokunywa pombe katika umri mdogo baada ya kubainika kuwa miongoni mwa waliofariki katika mkasa huo walikuwemo hata chipukizi wenye umri wa miaka 13. Familia za wahanga wa tukio hilo zinasema, hadi leo bado hazijabaini ni nini hasa kilisababisha vifo vya vijana wao.../