Somalia: Tuko tayari kuwapokea wakimbizi wa Dadaab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8782-somalia_tuko_tayari_kuwapokea_wakimbizi_wa_dadaab
Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia amesema nchi yake iko tayari kuwapokea raia wake kutoka kambi ya ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya, kwa shabaha ya kuwapa fursa wakimbizi hao kujenga taifa lao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2016 09:55 UTC
  • Somalia: Tuko tayari kuwapokea wakimbizi wa Dadaab

Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia amesema nchi yake iko tayari kuwapokea raia wake kutoka kambi ya ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya, kwa shabaha ya kuwapa fursa wakimbizi hao kujenga taifa lao.

Akiwahutubia waandishi wa habari pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika Ikulu ya Nairobi, Rais wa Somalia amesema serikali ya Mogadishu imeweka mikakati ya kutosha ya kuwapokea wakimbizi hao na kwamba mchakato huo utafanyika chini ya anga ya ubinadamu na ustaarabu. Amesema wakimbizi hao ni kiungo muhimu katika ujenzi wa taifa haswa kwa kuzingatia kuwa, wamepokea elimu ya viwango vya juu nchini Kenya. Kadhalika Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia ameishukuru Kenya kwa ukarimu wake, kwa kuwapa hifadhi wakimbizi hao kwa zaidi ya miongo miwili na nusu na kusisitiza kuwa wakati umefika kwa wakimbizi hao kurejea nyumbani na kujenga taifa. Awali serikali ya Somalia ilikosoa vikali azma ya Kenya ya kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab yenye mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Kisomali. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ya Mei 13 ilisema kuwa, kufungwa kwa kambi hiyo hakutakua na tija nyingine ghairi ya kuwasukuma wakimbizi hao kujiunga na makundi ya kigaidi kama vile al-Shaabab. Serikali ya Nairobi imesisitiza kwamba, inalazimika kuifunga kambi hiyo ya wakimbizi kutokana na mzigo mzito wa kiusalama, kiuchumi na masuala ya kimazingira.

Haya yanajiri huku nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais mwezi Agosti mwaka huu, licha ya mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.