Mkuu wa UNHCR azuru Kenya kujadili kurejeshwa nyumbani wakimbizi kutoka Somalia
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR Filippo Grandi yuko nchini Kenya ili kutathmini hali ya kambi ya wakimbizi ya Dadaab baada ya Kenya kuchukua uamuzi wa kufunga kambi hiyo yenye wakimbizi kutoka Somalia.
Grandi anatazamiwa kukutana na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kuhudhuria mkutano wa kusaini makubaliano kati ya nchi hiyo, Somalia na UNHCR kuhusu kurudishwa nyumbani wakimbizi wa Somalia.
Ziara yake imefanyika baada ya Kenya kutangaza kuwa itawarudisha Somalia wakimbizi zaidi 300,000 wanaoshi kwenye kambi ya Dadaab, mashariki kaskazini mwa Kenya.
Hiyo juzi, Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia alisema nchi yake iko tayari kuwapokea raia wake kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya, kwa shabaha ya kuwapa fursa wakimbizi hao kujenga taifa lao.
Akiwahutubia waandishi wa habari pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika Ikulu ya Nairobi, Rais wa Somalia amesema serikali ya Mogadishu imeweka mikakati ya kutosha ya kuwapokea wakimbizi hao na kwamba mchakato huo utafanyika chini ya anga ya ubinadamu na ustaarabu.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, kwa karibu miaka 25 sasa nchi hiyo imekuwa ikiwahudumia wakimbizi wapatao laki sita kutoka nchi jirani na hasa Somalia ambapo imegharamika pakubwa kiuchumi, kiusalama na kimazingira katika kuwadhaminia mahitaji yao ya kimsingi, jambo ambalo imesema haina tena uwezo wa kuendelea kulifanya.