Maelfu waandamana Tunisia kutaka rais Kais Saeid na serikali nzima wajiuzulu
Wapinzani na wakosoaji wa rais Kais Saeid wa Tunisia wamefanya maandamano makubwa wakimtaka kiongozi huyo na serikali ya sasa ya nchi hiyo wajiuzulu.
Mnamo Julai 25, 2021, Rais wa Kais Saeid, alipitisha maamuzi na kuchukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kutangaza kufuta mamlaka ya Bunge, kuondolewa kwa kinga ya wabunge, kumuuzulu waziri mkuu na kuvunja tume ya usimamizi wa katiba, hatua ambazo zilizusha mtafaruku na mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia, ambao uliambatana na wimbi la maandamano ya vyama na mirengo ya kisiasa, kikiwemo chama cha Kiislamu cha Ennahda.
Lakini mbali na hatua hizo, Julai 25, 2022, Saeid aliitisha kura ya maoni ya katiba mpya ambayo ilipitishwa licha ya kupigiwa kura na Watunisia wachache.
Wapinzani wanachukulia hatua za Rais wa Tunisia kuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba iliyoidhinishwa mwaka 2014 na mabadiliko ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa Zine El Abidine Ben Ali, lakini Saied mwenyewe anasisitiza kuwa hatua zake zimelenga kuiokoa Tunisia na msambaratiko wa kiuchumi na kijamii.../