Oct 16, 2022 11:33 UTC
  • 14 wauawa, kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan

Kwa akali watu watano wameuawa huku wengine tisa wakijeruhiwa katika mapigano mapya ya kikabila katika eneo la Kordofan Magharibi nchini Sudan.

Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na jeshi la Sudan inasema kuwa, ghasia hizo za kikabila baina ya jamii za Miseriya na Nuba zimetokea katika mji wa Lagawa katika jimbo la Kordofan Magharibi, lakini zimedhibitiwa na wanajeshi na askari polisi wa nchi hiyo.

Mapigano hayo yaliyotokea baina ya Ijumaa na jana Jumamosi ni sehemu ya wimbi jipya la uhasama na ghasia za kikabila zinazoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini (SPLM-N) ambayo wapiganaji wake wanatoka kabila la Nuba imekanusha madai ya kuchochea mapigano hayo, au kuwa na uhasama na watu wa kabila la Miseriya.

Wataalamu wanasema mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana, yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, yalizua ombwe la usalama ambalo limechochea kuibuka tena kwa ghasia za kikabila, katika nchi ambayo mapigano makali yanazuka mara kwa mara kuhusu ardhi, mifugo, upatikanaji wa maji na malisho.

Ramani ya Sudan na jirani yake Sudan Kusini

Julai mwaka huu, watu 79 waliuawa huku zaidi ya 200 wakijeruhiwa kutokana na ghasia za kikabila katika Jimbo la Blue Nile, kusini-mashariki mwa nchi.

Aidha mnamo Aprili, mapigano mengine ya kikabila yalipelekea kuuawa zaidi ya watu 200 katika eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan, ambalo hushudia vita na mapigano mara kwa mara.

Tags