Mahakama Afrika Kusini yakosolewa kwa kumuachia Mzungu katili
Uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba ya Afrika Kusini kumuachia huru raia mbaguzi wa Poland aliyekuwa akitumia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Chris Hani, mmoja wa viongozi waliokuwa wanapinga utawala wa zamani wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini (apartheid).
Limpho Hani, mjane wa mwaharakati huyo wa kupinga mfumo wa apartheid nchini Afrika Kusini amesema amesikitishwa na hukumu hiyo ya kumuachia huru Janusz Walus, raia mbaguzi wa Poland.
Amesema, "Mahakama hii haijzingatia kadhia ya wahanga. Nchi hii imekwisha. Raia wa kigeni Mzungu anaweza kuja hapa nchini, amuue mume wangu na kisha mahakama inapuuza matatizo na msongo wa mawazo iliyoupitia familia yangu."
Akisoma uamuzi huo jana Jumatatu, Jaji Mkuu Raymond Zondo amepuuzilia mbali uamuzi uliotolewa na Waziri wa Sheria na Masuala ya Magereza, na ameamua kumuachia huru Walus kwa sharti kuwa atumikie kifungo cha nyumbani kwa siku 10.
Kadhalika Chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini kimekosoa vikali uamuzii huo wa Mahakama ya Katiba kumuachia huru raia huyo wa Poland mwenye misimamo ya kibaguzi. Hani alikuwa kiongozi wa chama hicho ambacho kina ukurub na chama tawala ANC.
Janusz Walus alihamia Afrika Kusini mwaka 1981 na alikuwa muungaji mkono mkubwa wa mfumo usio wa kibinadamu wa Apartheid. Alitekeleza ukatili huo mwaka 1993, kitendo ambacho nusra kiitumbukieza Afrika Kusini katika vita vya ndani.
Mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid ambao ni miongoni mwa sura za ukatilii na unyama wa kutisha na ubaguzi wa kizazi uliotawala Afrika Kusini kwa miaka mingi kwa maslahi ya wazungu waliowachache dhidi ya wazalendo weusi, ulifutwa rasmi nchini humo mwaka 1991.
Raia mbaguzi wa Poland alihukumiwa kunyongwa mwaka 1993, lakini hukumu hiyo iliangalia upya baadaye na korti ya Afrika Kusini ikaamua kumfunga maisha jela.