Upinzani wataka Rais wa Tunisia ajiuzulu kwa 'kususiwa' uchaguzi wa bunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91840-upinzani_wataka_rais_wa_tunisia_ajiuzulu_kwa_'kususiwa'_uchaguzi_wa_bunge
Muungano mkubwa zaidi wa upinzani nchini Tunisia umemtaka Rais Kais Saied wa nchi hiyo ajiuzulu kutokana na ushiriki mdogo wa wananchi katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 18, 2022 07:11 UTC
  • Upinzani wataka Rais wa Tunisia ajiuzulu kwa 'kususiwa' uchaguzi wa bunge

Muungano mkubwa zaidi wa upinzani nchini Tunisia umemtaka Rais Kais Saied wa nchi hiyo ajiuzulu kutokana na ushiriki mdogo wa wananchi katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jana.

Taarifa ya muungano huo wa vyama vya upinzani nchini Tunisia imesema, Rais Kais Saied amepoteza uhalali wa kuendelea kuwa kiongozi wa nchi hiyo, baada ya Watunisia wengi kususia uchaguzi huo.

Nejib Chebbi, kiongozi wa Muungano wa Uokovu amesema, matokeo ya awali yanaonesha kuwa, licha ya wananchi milioni 9.3 kutimiza masharti ya kushiriki katika uchaguzi huo ili kuwachagua wabunge 161 kati ya wagombea  1058, lakini ni asilimia 9 tu waliojitokeza kushiriki zoezi hilo.

Amesema, "Kilichofanyika leo (jana Jumamosi) ni zilzala. Tokea sasa, hatumtabui Saied kama rais halali (wa Tunisia) na tunamtaka ajiuzulu mara moja kufuatia mtikisiko huo." 

Wananchi wa Tunisia jana Jumamosi walipiga kura katika uchaguzi wa kwanza wa wabunge tangu Rais Kais Saied atangaze  mnamo Julai 25 mwaka jana kulisimamisha Bunge na kutwaa madaraka yote ya nchi. 

Rais Kais Saied (Kulia) wa Tunisia inayokabiliwa na mgogoro

Vyama 12 vya siasa kikiweko chama cha Kiislamu cha Ennahdha na kile cha mrengo wa kulia cha Qalb Tounes ambavyo kwa pamoja vilikuwa vikiunda muungano mkubwa katika bunge lililovunjwa, vimetangaza kususia uchaguzi huo wa bunge.

Wakati huo huo Jumuiya ya Wafanyakazi yenye nguvu ya Tunisia (UGTT) pia imesema inapinga muundo huo wa uchaguzi kwa ujumla.