Jeshi la Somalia lakomboa mji wa kistratejia katika ngome ya al-Shabaab
Vikosi vya serikali ya Somalia vimefanikiwa kuukomboa mji wa kistratejia wa Harardhere, moja ya ngome za kundi la kigaidi la al-Shabaab karibu na Bahari Hindi.
Taarifa ya Jeshi la Somalia (SNA) imesema, wanajeshi wa nchi hiyo waliuteka mji huo mapema Jumatatu katika mji huo wa Pwani ulioko katika eneo la Mudug, jimbo la Galmudug, yapata kilomita 491 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.
Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Abdulkadir Mohamed Nor amethibiti habari ya kukombolewa mji wa Haradhere, saa chache baada ya jeshi la Somalia kukomboa mji mwingine wa kistratejia wa Galcad, jimbo la Galmudug.
Rais wa jimbo la Galmudug, Ahmed Abdi Karie Qoorqoor amesema: Tunavipongeza vikosi vya SNA kwa kupiga hatua kwenye operesheni dhidi ya al-Shabaab mashariki mwa eneo la Galgaduud, na mji wa Galcad.
Mwishoni mwa mwezi uliomalizika wa Disemba, mashambulizi ya Jeshi la Somalia (SNA) dhidi ya kundi la magaidi wa al-Shabaab yalipata mafanikio mapya baada ya vikosi vyake kuukomboa mji mwingine wa Runirgoud, ngome ya mwisho ya magaidi hao wakufurishaji huko Shabelle ya Kati, takriban kilomita 240 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.
Mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kuhusishwa na wanamgambo wanaounga mkono serikali ambao ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na magaidi wa al-Shabaab.