Lavrov atetea maneva ya baharini na Afrika Kusini akiwa ziarani nchini humo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kwamba Moscow haitaki kile alichokiita “chokochoko” zozote kuhusu mazoezi ya pamoja ya majeshi ya majini kati ya nchi hiyo, China na Afrika Kusini yaliyopangwa kufanyika mwezi ujao.
Sergei Lavrov amebainisha hayo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa ziarani nchini Afrika Kusini jana Jumatatu wakati akijibu lawama na ukosaji kuhusiana na maneva hayo. Afrika Kusini ni moja ya nchi waitifaki muhimu wa Russia katika bara la Afrika; bara ambalo nchi zake zimegawanyika na kuwa na misimamo tofauti sasa kufuatia uvamizi wa Russia huko Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, nchi yake tayari imetoa taarifa zote za lazima kuhusiana na mipango ya maneva hayo ya baharini ya kijeshi kati ya nchi hiyo, China na Afrika Kusini.
Sergei Lavrov jana Jumatatu alikutana na kuzungumza mjini Pretoria Afrika Kusini na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo bi Naledi Pandor. Maafisa wa serikali ya Afrika Kusini wameitaja ziara hiyo ya Lavrov nchini humo kuwa ni ya kawaida lakini ambayo haijapewa uzito na baadhi ya vyama vya siasa na jamii ndogo ya raia wa Ukraine waishio nchini Afrika Kusini.
Serikali ya Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini haijaegemea upande wowote katika vita vinavyoendelea huko Ukraine na imeeleza nia yake ya kuwa tayari kupatanisha mgogoro wa sasa kati ya Russia na Ukraine. Wakati huo huo Naledi Pandor Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa nchi yake haitaburuzwa katika kuunga mkono upande wowote na imezikosoa nchi za Magharibi kwa kuishutumu Russia huku zikipuuza hatua nyingine za uvamizi na kichokozi kama mashambulizi yanayofanywa kila siku na ukaliaji mabavu wa utawala wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Nchi zote mbili yaani Russia na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana kibiashara kwa miaka kadhaa sasa huku uuzaji wa bidhaa mbalimbali na biashara za Afrika Kusini nchini Russia zikifikia kiasi cha dola milioni 587 mwaka 2020 na uuzaji wa bidhaa za Russia nchini Afrika Kusini ukifikia thamani ya dola milioni 506.
Jeshi la majini la Afrika Kusini linajiandaa kuwa mwenyeji wa maneva ya baharini ya pamoja kati yake na Russia na China yaliyopangwa kufanyika katika pwani ya nchi hiyo kuanzia Februari 17 hadi 27 mwaka huu; hatua ambayo inaweza kuvuruga zaidi uhusiano wake na Washington na nchi za Ulaya. Meneva hayo yamesadifiana na kumbukumbu ya kwanza tangu Russia ianzishe oparesheni ya kijeshi dhidi ya Ukraine mnamo Februari 24 mwaka jana.