Mkutano wa kujadili vita dhidi ya Al-Shabaab wafanyika Somalia
(last modified Thu, 02 Feb 2023 02:09:58 GMT )
Feb 02, 2023 02:09 UTC
  • Mkutano wa kujadili vita dhidi ya Al-Shabaab wafanyika Somalia

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia jana Jumatano alikuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa nchi kadhaa jirani uliofanyika kwa lengo la kujadili mikakati ya kikanda ya kupambana na wanamgambo wa kundi la al Shabaab lenye makao yake huko Somalia.

Mkutano huo wa Mogadishu umehudhuriwa na Rais William Ruto wa Kenya, Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. Viongozi hao wanne wamejadili suala la kuunganisha juhudi dhidi ya kundi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Kundi la al Shabaab limekuwa likifanya hujuma na mashambulizi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa zaidi ya miaka 15 sasa. 

Ulinzi mkali uliimarishwa mjini Mogadishu ikiwa ni pamoja na kusitishwa safari zote za ndege za kibiashara kuelekea Mogadishu. 

Baada ya kuanza kazi mwezi Mei mwaka jana, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia alitangaza vita vya pande zote dhidi ya wanamgambo wa al Shabaab na kuwatolea wito wananchi wa Somalia kusaidia juhudi za serikali ili kulisambaratisha kundi hilo la kigaidi. 

Wanamgambo wa al Shabaab 

Katika miezi ya karibuni, jeshi na wanamgambo wa makundi ya kikoo ya Somalia walifanikiwa kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametekwa na al Shabaab katika oparesheni iliyotekelezwa kwa usaidizi wa  kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika (ATMIS).

Mawaziri wa Ulinzi na Wakuu wa Usalama wa nchi nne hizo Jumanne iliyopita walikutana mjini Mogadishu kuandaa mkutano wa jana. Serikali ya Somalia imesema kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kuwa chachu ya kukombolewa haraka maeneo yote ya Somalia kutoka kwenye makucha ya wanamgambo ambao wamepata pigo kubwa katika medani ya vita katika wiki chache zilizopita."

Wanamgambo wa kundi la al Shabaab wanaendelea kufanya hujuma na harakati zao katika maneo ya ndani ya Somalia na katika nchi jirani.