Afrika Kusini yatangaza hali ya maafa kufuatia kukatika umeme
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i93882-afrika_kusini_yatangaza_hali_ya_maafa_kufuatia_kukatika_umeme
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye amekabiliwa na lawama na ghadhabu za wananchi, jana alitangaza "hali ya maafa nchini humo kufautia kukosekana huduma ya umeme na kuahidi kumaliza shida ya upungufu wa nishati ambayo inatishia utulivu wa kiuchumi na kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2023 03:26 UTC
  • Afrika Kusini yatangaza hali ya maafa kufuatia kukatika umeme

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye amekabiliwa na lawama na ghadhabu za wananchi, jana alitangaza "hali ya maafa nchini humo kufautia kukosekana huduma ya umeme na kuahidi kumaliza shida ya upungufu wa nishati ambayo inatishia utulivu wa kiuchumi na kisiasa nchini humo.

Huku Afrika Kusini ikistahimili kukatika kwa umeme kila siku kwa hadi masaa 10, Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo jana Alhamisi alitangaza "hali ya maafa" nchini kote ili kushughulikia shida ya umeme iliyoiathiri nchi hiyo. Imeelezwa kuwa biashara mbalimbali zimeathirika kwa kukosa umeme huku vifaranga wa siku moja wakifa kwa baridi, wamiliki wa maduka makubwa wanakimbilia kuuza nyama kabla ya kuharibika na biashara nyingi zimelazimika kufungwa.

Tatizo la kukatika umeme nchini Afrika Kusini linatajwa kusababishwa na mitambo chakavu katika vituo vya umeme vinavyotumia makaa ya mawe; ambavyo Kampuni ya Umeme ya serikali ya Afrika Kusini isiyofanya kazi Eskom inafanya kila njia ili kuhuisha utendaji wake.   

Afrika Kusini na tatizo la kukatika umeme 

Kukatika kwa umeme kumekuwa sehemu ya maisha nchini Afrika Kusini kwa karibu miaka 16 sasa, lakini miezi kadhaa iliyopita nchi hiyo imekumbwa na tatizo kubwa la kusalia gizani bila ya huduma ya umeme.

Akihutubia taifa jana kwa njia ya televisheni, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema: tunatangaza janga la kitaifa ili kukabiliana na mgogoro wa umeme na madhara yake." Wananchi wa Afrika Kusini wanataka kuchukuliwa hatua za kivitendo katika uwanja huo.

Hii ni katika hali ambayo, wapinzani wa kisiasa na mashirika ya kiraia Afrika Kusini wamefanya maandamano makubwa mitaani na kuiburuza serikali mahakamani kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwani kukatika huko kwa umeme kumevuruga biashara, elimu na huduma za afya nchini.