Jeshi la Somalia latoa pigo jingine kwa al-Shabaab, laua 117 Mudug
Idadi kubwa ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la Mudug jimboni Galmudug, katikati nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hayo yalisemwa jana na Jenerali Mohamed Tahalil Bihi, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) ambaye ameongeza kuwa, mbali na magaidi 117 kuuawa, wanachama wengine wengi wa genge hilo wamejeruhiwa katika operesheni hiyo ya masaa manane mwishoni mwa wiki.
Amesema kuangamizwa magaidi 117 katika operesheni hiyo katika mji wa Doonyale jimboni Galmudug ndiyo mafanikio makubwa zaidi ya jeshi la Somalia dhidi ya genge hilo la ukufurishaji tangu mwaka huu 2023 uanze katika eneo hilo.
Bihi ameongeza kuwa, al-Shabaab wamepoteza miji mingi ya kistaratajia iliyokuwa mikononi mwao katika eneo la Mudug, na kwamba vikosi vya serikali vikishirikiana na askari wa kujitolea wataendeleza operesheni hizo za kulitokomeza kabisa genge hilo la kigaidi.
Mwishoni mwa Januari mwaka huu, wanachama 136 wa al-Shabaab, wakiwemo makamanda 3 wa gege hilo waliangamizwa kwenye operesheni nyingine katika eneo la Lower Shabelle.
Tangu 2007, kundi la al Shabaab limekuwa likipigana na serikali ya shirikisho inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa ya Somalia, na baada ya wapiganaji wake kufukuzwa kutoka miji mikuu wa nchi hiyo kati ya 2011 na 2012, limejikita zaidi katika maeneo ya vijijini.