Mar 19, 2023 12:39 UTC
  • Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lafanyika visiwani Zanzibar, Tanzania

Kongamano la siku mbili la Idhaa za Kiswahili Duniani limeendelea leo visiwani Zanzibar nchini Tanzania kwa mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu wa lugha hiyo kutoka pembe tofauti za dunia.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) kwa kushirikiana na wadau wengine, limewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa na wadau wengine wa lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na Vyuo Vikuu.

Katika hotuba ya ufunguzi wa kongamano hilo hapo jana, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi aliwahutubu washiriki akisema: "wito wangu kwa washiriki wa kongamano hili, mtumie vyema taaluma mtakayoipata; na bila ya shaka mtajifunza mambo mengi yanayohusu Kiswahili, utangazaji na uandishi wa habari. Ninaamini kwamba wataalamu walioandaliwa, watatoa taaluma muhimu ya matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili itakayokuongezeeni umahiri na kukujengeeni uwezo zaidi”.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo ni "Changamoto za Matumizi ya Kiswahili katika kazi ya utangazaji ndani ya vituo vituo vya kazi". Mwasilishaji wa mada hiyo Edith Nibhakwe, mwanahabari kutoka nchini Rwanda amezungumzia kuhusu namna ambavyo upana wa ufikiaji lugha fulani unavyoweza kuathiri kwa uchanya au uhasi katika kupigania haki za msichana na mwanamke hasa katika nchi kadhaa zenye lugha tofauti na akasema, “kwa mfano ninapotoa mafunzo kuhusu haki za wanawake nikitumia Kinyarwanda, nikitumia Kirundi au Kiganda mafunzo yangu yatawafikia watu wachache, lakini tukiweza kuwasiliana katika lugha pana ya Kiswahili ninaweza nikawafikia watu wengi.”

Itakumbukwa kuwa mwaka 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, liliitambua lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha za kimataifa na takwimu zinaonesha kuwa Kiswahili ndio lugha ya Kibantu yenye wazungumzaji wengi zaidi barani Afrika.../

Tags