Afrika Kusini yawafurusha wanaotafuta hifadhi waliopiga kambi nje ya ofisi ya UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96526-afrika_kusini_yawafurusha_wanaotafuta_hifadhi_waliopiga_kambi_nje_ya_ofisi_ya_un
Polisi nchini Afrika Kusini imewafurusha raia wanaotafuta hifadhi zaidi ya 100 waliokuwa wamepiga kambi kwa zaidi ya miaka mitatu nje ya ofisi za Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR mjini Pretoria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2023 22:09 UTC
  • Afrika Kusini yawafurusha wanaotafuta hifadhi waliopiga kambi nje ya ofisi ya UN

Polisi nchini Afrika Kusini imewafurusha raia wanaotafuta hifadhi zaidi ya 100 waliokuwa wamepiga kambi kwa zaidi ya miaka mitatu nje ya ofisi za Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR mjini Pretoria.

Watafuta hifadhi hao walianza kuishi kwenye mahema waliyoyasimika nje ya ofisi za UNHCR; huku wakitaka kuhamishiwa katika nchi nyingine baada ya kujiri mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni huko Afrika Kusini mwaka 2019. 

uongozi wa Manispaa ya Pretoria wiki iliyopita ulipata kibali kutoka Mahakama Kuu cha kuwaondoa sehemu walipopiga kambi raia hao wa kigeni; ambapo jana Ijumaa polisi ya Afrika Kusini ilitekeleza zoezi hilo.  

Nyaraka kutoka Mahakama Kuu ya Afrika Kusini zimeeleza kuwa wakimbizi wataondolewa mbele ya ofisi ya UNHCR  na kupelekwa katika kituo cha kituo cha muda cha kuhifadhi wahamiaji wasio na vibali ambao wametengwa kwa ajili ya kurejeshwa katika nchi zao za asili.

Makumi ya maafisa polisi huko Pretoria walitekeleza zoezi hilo la kuwaondoa raia hao wa kigeni kwa kusaidiwa na ofisi za uhamiaji na nyinginezo. Kobus Meijer Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Afrika Kusini aliwaonya hiyo jana raia hao wa kigeni kwamba watakamatwa na kuzuiliwa iwapo watakataa kuondolewa na polisi.

Watafuta hifadhi raia wa kigeni nchini Afrika Kusini 

Wakati huo huo Laura Padoan Msemaji wa UNHCR amezihimiza mamlaka husika nchini Afrika Kusini kuendesha zoezi hilo kwa amani na kuhakikisha kuwa zinaamiliana kwa ubinaadamu, kwa heshima na adamu na familia mbalimbali za raia hao wa kigeni.