Shambulio la watu wenye silaha kusini magharibi mwa Sudan
Watu waliokuwa na silaha wamewaua watu kadhaa na kuwajeruhi wengine baada ya kushambulia eneo moja kusini magharibi mwa Sudan.
Watu wasiopungua 5 wameuawa na wengine 13 wamejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika eneo la Tour katika jimbo la Darfur ya Kati huko kusini magharibi mwa Sudan.
Watu walioshuhudia wameeleza kuwa mamia ya wakazi wa eneo la Tour wamezihama nyumba zao na kukimbilia msituni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatima ya watoto wengi ambao wamehama makazi yao katika eneo hilo lililokabiliwa na shambulio la watu wenye silaha haifahamiki . Jimbo la Darfur huko Sudan tangu mwaka 2003 limekuwa likikumbwa na hali ya mchafukoge na mapigano ya silaha kati ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi na vile vile mizozo ya kikabila.