Mafuriko yauwa watu 7 Afrika Kusini; watu wengine kadhaa hawajulikani walipo
Mamlaka ya serikali za mitaa nchini Afrika Kusini Ijumaa hii zimetangaza kuwa watu saba wameaga duunia na wengine saba hawajulikani walipo baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko ndani na nje ya mji wa Durban.
Serikali ya jimbo la Kwa Zulu-Natal imetangaza kuwa watu sita wamepoteza maisha Durban na mmoja huko Port Sheptsone, mji wa ufukweni umbali wa kilomita 120 kusini kwa mji wa Durban. Maafisa husika wa mji wa Durban wameeleza kuwa miili ya mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 na wa binti mmoja imekutwa mferejini baada ya kusombwa na mafuriko huko Durban.
Nyumba zisizopungua 70 pia zimeanguka na nyingine zaidi ya 100 zimeathiriwa na mafuriko. Wakati huo huo watu zaidi ya 150 wamelazimika kuhama makazi yao. Baadhi ya watu sasa wanaishi katika madarasa ya shule huko Kwa Zulu-Natal na katika majengo mengineyo.
Mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zimeiathiri Afrika Kusini huku hali ya hewa isiyo ya kawaida ikisababisha kimbunga kinachojulikana kwa jina la "Landspout". Idara ya Hali ya Hewa ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, upepo mkali katika viunga vya mji wa Durban umerekodiwa kuvuma kwa kasi ya zaidi ya maili 100 kwa saa.