Watu wasiopungua 16 wapoteza maisha katika mkasa wa kuvuja gesi Afrika Kusini
Watu wasiopungua 16 wakiwemo watoto wameaga dunia baada ya kuvuja gesi katika eneo la mabanda karibu na mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Mkasa huo uliotokea jana usiku unakisiwa kusababishwa na shughuli haramu za uchimbaji madini zinaofanywa katika makazi yasiyo rasmi ya Angelo karibu na wilaya ya Boksburg mashariki mwa Johannesburg.
William Ntladi, msemaji wa Kitengo cha Huduma za Dharura ameeleza kuwa, hadi sasa watu 16 wamethibitishwa kupoteza maisha na kwamba madaktari wamefanikiwa kuokoa baadhi ya watu huku wengine wakipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Watu wanne kati ya waliofikishwa hospitali wameriporiwa kuwa mahututi huku wanawake watano na watoto watatu wakiwa miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika tukio hilo la kuvuja gesi. Idara ya Huduma za Dharura imeeleza kuwa baada ya kufikia eneo la tukio imegundua kwamba ilikuwa na gesi iliyovuja kutoka katika silinda iliyokuwa na gesi ya sumu.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa, gesi hiyo ilikuwa ikitumika kama sehemu ya shughuli haramu za uchimbaji madini katika eneo hilo la mabanda la watu maskini.
Huku kukiwa na kiwango kikubwa cha watu wasio na ajira cha zaidi ya asilimia 32, Afrika Kusini inatambuliwa kuwa nchi ya maelfu ya wachimba migodi haramu wanaoitwa "Zama Zamas". Neno hili lina maana ya "Wale wanaojaribu bahati zao" kwa lugha ya Kizulu.