Aug 12, 2024 05:17 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Agosti 12

Hujambo msikilizaji mpenzi na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyoshuhidiwa kote duniani ndani ya siku saba zilizopita…..

Iran yazoa medali lukuki Michezo ya Olimpiki ya Paris

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya 21 duniani na ya 5 barani Asia kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris iliyofunga pazia lake Jumapili ya Agosti 11 nchini Ufaransa. Wanamichezo wa Iran wamezoa jumla ya medali 12, zikiwemo 3 za dhahabu, 6 za fedha na 3 za shaba. Dhahabu ya tatu ya Iran ilitwaliwa na Arian Salimi baada ya kuibuka kidedea kwenye fainali ya taekwondo, kategoria ya uzani mzito kwa wanaume wenye kilo zaidi ya 80.

Mwanataekwondo wa Iran, Arian Salimi aliyeshinda medali ya dhahabu

Aliibuka mshindi baada ya kumchakaza Muingereza, Caden Cunningham katika pambano la aina yake Jumamosi usiku.  Dhahabu nyingine 2 za Iran zilitiwa kibindoni na Saeed Esmaeili kwenye mieleka ya jadi mtindo wa Greco-Roman kwa wanamieleka wenye kilo 67, na Mohammad-Hadi Saravi wa wanamieleka wenye kilo 97. Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amewanyooshea mkono wa pongezi wanamichezo wote wa Jamhuri ya Kiislamu walioshiriki na kushinda medali tofauti na kupaisha jina la Iran kwenye jukwaa hilo la kimataifa nchini Ufaransa.

Dondoo za Olimpiki

Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana alitangaza Ijumaa alasiri kuwa sikukuu ya kusherehekea ushindi wa Letsile Tebogo, ambaye siku ya Alkhamisi aliandika historia ya kutwaa medali ya kwanza ya dhahabu kwa nchi hiyo katika mbio za mita 200. Mwanariadha huyo ameingia katika kumbukumbu za historia kwa kuwa Mwafrika wa kwanza kushinda mbio hizo za Olimpiki za mita 200. Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 21 aliwapiku wapinzani wake Kenny Bednarek na Noah Lyles wa Marekani, na kumaliza kwa kutumia sekunde kwa sekunde 19.46, na kushinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki ya Botswana huko Paris. Pia ilikuwa dhahabu ya kwanza kabisa kwa Botswana tangu nchi hiyo ianze kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 1980. Kamati ya Olimpiki Duniani, serikali na mashirika mbali mbali ya Botswana yamemtumza zaidi ya dola 15,000 pamoja na nyumba.  

Baadhi ya wanariadha wa Afrika waliofanya vyema kwenye Michezo ya Paris

Kwengineko, Kenya Jumapili ilifunga duru ya 33 ya Michezo ya Olimpiki kwa nishani ya shaba kupitia kwa bingwa wa Boston Marathon, Hellen Obiri mjini Paris. Binti huyo mwenye miaka 34 alikamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa kutumia saa 2:23:10, nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan (2:22:55) na mshikilizi wa rekodi ya dunia Tigst Assefa kutoka Ethiopia (2:22:58) walionyakua dhahabu na fedha, mtawalia. Mbali na kuibuka bingwa mpya wa Olimpiki, Sifan Hassan pia aliweka rekodi mpya ya Olimpiki ya marathon ya wanawake baada ya kufuta ile ya saa 2:23:07 iliyowekwa mwaka 2012 na Muethiopia Tiki Gelana.

Jumamosi bingwa wa Tokyo Marathon Benson Kipruto aliishindia Kenya medali ya shaba katika mbio za masafa marefu za Michezo ya Olimpiki mjini Paris kwa upande wa wanaume. Kipruto alikamilisha mbio hizo kwa saa 2:07:00. Bingwa wa 2016 na 2021 Eliud Kipchoge aliyekuwa akifukuzia kutetea taji na kuwa mtimkaji wa kwanza kabisa mwanamume kutawala marathon mara tatu mfululizo kwenye Olimpiki alishindwa kumaliza mbio hizo, na ametangaza rasmi kustaafu Olimpiki. Muethiopia Tamirat Tola aliibuka mshindi kwa rekodi mpya ya Olimpiki ya saa 2:06:26 baada ya kufuta rekodi ya mwendazake Samuel Wanjiru wa Kenya ya saa 2:06:32 iliyodumu tangu 2008. Mbelgiji Bashir Abdi aliyepata nishani ya shaba mjini Tokyo nchini Japan mwaka 2021, aliridhika na medali ya fedha kwa kumaliza wa tatu kwa kutumia saa 2:06:47. Mshindi namba tano wa mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto mwaka 2016 jijini Rio de Janeiro, Mtanzania Alphonce Felix Simbu ameshindwa kutamba kwenye Olimpiki ya mwaka huu jijini Paris, baada ya kumaliza nafasi ya 17 kwenye mbio ndefu za wanaume akitumia muda wa saa 2:10:03.

Mwanariadha nyota wa Kenya, Eliud Kipchoge hakuwa na bahati mjini Paris

Tanzania kwa mara nyingine imetoka kapa kwenye mashindano hayo makubwa yanayojumuisha michezo mbalimbali. Aidha mwanariadha nyota wa Kenya, Faith Kipyegon amethibitisha kuwa simba jike katika mbio za mita 1,500 duniani baada ya kuandikisha historia ya kuwa wa kwanza kabisa kuzoa dhahabu tatu mfululizo za Olimpiki, jijini Paris, Ufaransa. Jumamosi usiku, afande Kipyegon alionyesha ujasiri mkubwa kwa kufyatuka kama mshale alipopiga kona ya mwisho na kutwaa taji kwa rekodi mpya ya Olimpiki ya dakika 3:51.29. Kipyegon, 30, alishikilia rekodi ya awali ya Olimpiki aliponyakua taji lake la pili katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara nne; dakika 3:53.11 jijini Tokoyo, Japan, mwaka 2021. Bingwa wa dunia mbio za mita 800 za chipukizi wasiozidi miaka 20 mwaka 2021, Emmanuel Wanyonyi, sasa pia ni bingwa wa Olimpiki baada ya kuponyoka na taji kwa dakika 1:41.19 jijini Paris, Ufaransa, Jumamosi usiku. Wanyonyi,20, ni mshindi wa 800m mwenye umri mdogo kabisa tangu Olimpiki zianzishwe mwaka 1896.

Kenya imelitoa kimasomaso bara Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya 17, kwa kuzoa medali 11, zikiwemo 4 za dhahabu, 2 za fedha na 5 za shaba. Marekani imemaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mashindano hayo baada ya kuchota jumla ya medali 126, zikiwemo 40 za dhahabu, ikifuatia na China yenye medali 91 zikiwemo dhahabu 40, huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Japan iliyozoa medali 45, zikiwemo 20 za dhahabu. Mwenyeji Ufaransa pamoja makeke yote imemaliza ya tano kwa dhahabu 16, nyuma ya Australia iliyobeba medali 18 za dhahabu.

Mbali na hayo, timu ya taifa ya soka ya Uhispania ilimcharaza mwenyeji Ufaransa mabao 5-3 kwenye mechi ya fainali ya kuwania ubingwa wa taji la Olimpiki. Katika mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Parc des Princes Ijumaa, licha ya Ufaransa kutoka nyuma kwa kuzabwa mabao 3-1 na kusawazisha, lakini walishindwa kutamba kwenye dakika za nyongeza na kuishia kugaragazwa mabao 5-3 na Uhispania.

Ngao ya Jamii Tanzania; Yanga yaiadhibu Azam

Yanga imetwaa Ngao ya Jamii ya Tanzania ya 2024 baada ya kuicharaza Azam mabao 4-1. Timu hizo zimekutana tena miezi 2 baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho iliyomalizika kwa sare ya 0-0. Mtanange huu wa Ngao ya Jamii sio tu pambano la kawaida, bali ni mchezo wenye historia na hisia kali.

Wanasema ni zaidi ya mechi ya ufunguzi wa msimu; ni mechi ya kisasi, ubabe, na utemi katika ulimwengu wa soka nchini Tanzania, na ndio maana Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili ulifurika furi furi kushuhudia mchuano huo, ambapo Wananchi waliibuka kidedea.

Ngao ya Jamii Uingereza; City yaipepeta Man U

Huko Uingereza, klabu ya Manchester City ilimetwaa Ngao ya Jamii ya mwaka huu, baada ya kumzaba mtani wake wa jadi, Manchester United kkwenye upigaji matuta, baada ya kutoshana nguvu kwa kulimana 1-1 katika dakika za ada na nyongeza. 

 

Tags