Ulimwengu wa Spoti, Jan 12
https://parstoday.ir/sw/news/event-i135396-ulimwengu_wa_spoti_jan_12
Natumai mambo yako yanakuendea shwari msikilizaji mpenzi, na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.
(last modified 2026-01-21T02:33:43+00:00 )
Jan 12, 2026 06:37 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 12

Natumai mambo yako yanakuendea shwari msikilizaji mpenzi, na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Mieleka: Iran mshindi wa 2 Uturuki

Timu ya mieleka aina ya Greco-Roman ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika mashindano ya mieleka ya Yasar Dogu na Vehbi Emre ya 2026 nchini Uturuki. Mashindano hayo ya kimataifa yalifanyika Antalya, Uturuki kuanzia Januari 8 hadi 10. Wairani Arman Tahmasebi katika safu ya wanamieleka wenye kilo 130 na Amir Reza Moradian katika kategoria ya kilo 97, walishinda medali ya dhahabu kila mmoja katika mapambano yao ya fainali.

Timu ya mieleka aina ya Greco-Roman ya Iran

 

Wairani wengine, Ali Hajivand katika kilo 63 na Mohammad Arjmand katika kilo 82 waliishindia Jamhuri ya Kiislamu medali mbili za fedha. Medali za shaba za timu ya mieleka ya Greco-Roman ya Iran zilitwaliwa na Kianoush Shamshiri na Mehdi Kamali katika kilo 55, Mohammad Ashiri katika kilo 60, Mohammad Eskandari katika kilo 67 na Ali Asghar Sam Daliri katika kilo 77.

AFC: Iran sare na Uzbekistan

Timu za soka za vijana za Iran na Uzbekistan wikendi zilitoka sare ya bila kufungana kwenye mchuano wa Kombe la Asia la AFC kwa vijana wenye chini ya miaka 23 la 2026. Korea Kusini iliizaba Lebanon mabao 4-2 mapema siku hiyo. Iran ilikuwa imeanza kampeni kwa sare ya 0-0 dhidi ya Korea Kusini Jumatano.

Timu ya soka ya mabarobaro ya Iran

 

Timu hiyo ya mabarobaro ya Iran inatazamiwa kushuka simbani kuvaana na Lebanon Jumanne hii katika mchezo mwingine wa Kundi C ambao ni lazima washinde iwapo wanataka kusogea mbele. Mashindano hayo ya kandanda ya vijana wa Asia yalianza Januari 6 huko Riyadh, Saudi Arabia na yanatazamiwa kufunga pazia lake Januari 24.

AFCON: Miamba nje

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025 inaelekea kufikia tamati, ambapo baadhi ya miamba ya soka barani Afrika imebanduliwa, huku baadhi ya vibonde wakitinga nusu fainali kimuujiza. Hatua ya robo fainali ya michuano ya AFCON imekamilika na sasa macho yote yameelekezwakwenye michezo ya nusu fainali itakayofanyika Jumatano Januari 14. Mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah alifanikiwa kucheka na nyavu wakati timu yake ya taifa ya Misri ikiwafungisha virago mabingwa watetezi, Ivory Coast, na kutinga nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa ushindi wa mabao 3-2.

Mshambuaji mahiri wa Misr na Liverpool, Mohammed Salah 

 

Mo Salah alifunga bao lake la nne katika michuano hiyo - bao la tatu kwa Misri katika mchezo huo - katika dakika ya 52 ya pambano la kukata na shoka la Jumamosi, na Mafarao walilihitaji bao hilo, kwani Ivory Coast ilitishia kuwa kifua mbele tena, kwa mara ya pili kwenye mechi hiyo. Misri, hata hivyo, iliendelea kupambana kufa kupona licha ya mashinikizo makubwa ya Ivory Coast, na kukata tiketi ya kucheza nusu fainali na mabingwa wa 2021 Senegal mjini Tangier siku ya Jumatano. Misri wanafukuzia taji la nane la AFCON. Mambo yalikuwa hivi mjini Agader.

Kwengineko, Nigeria ilifanikiwa kuvuna ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Algeria katika robo fainali nyingine ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Victor Osimhen na Akor Adams na kutinga nusu fainali, ambapo watawajihiana na wenyeji Morocco. Osimhen alifunga krosi ndefu kutoka upande wa kushoto wa Bruno Onyemaechi dakika mbili za kipindi cha pili siku ya Jumamosi huku kipa wa Algeria, Luca Zidane akiruka mithili ya tumbili kujaribu kuzuia bao, lakini akaishia kuukosa mpira na kuruhusu bao rahisi. Adams aliongeza bao la kuongoza la Nigeria dakika 10 baadaye, huku Osimhen akimlisha mpira bila ubinafsi, na akauchukua karibu na Zidane kabla ya kuuweka kwenye wavu tupu. Ulikuwa mchezo wa kuvutia wa Nigeria, ambao miezi miwili iliyopita walikosa kufuzu kwa Kombe la Dunia, walipowalemea wapinzani wao tangu mwanzo kwenye Uwanja wa Grand Stade de Marrakesh, wakionekana kudhamiria zaidi, wepesi zaidi uwanjani na wenye nguvu zaidi.

Algeria walikuwa wamelazimishwa kucheza muda wa ziada kabla ya kushinda mchuano wao wa hatua ya 16 bora dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumanne. Kinyume chake, Nigeria walipata ushindi mzuri wa mabao 4-0 dhidi ya Msumbiji Jumatatu. Super Eagles sasa watamenyana na Morocco mjini Rabat katika nusu fainali nzito siku ya Jumatano.

Kombe la AFCON

 

Huku hayo yakiarifiwa, mshambulizi aliyerejea kikosini, Iliman Ndiaye alitikisa nyavu katika kipindi cha kwanza na kuipa Senegal ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mali iliyokuwa na wachezaji 10 mjini Tangier, mnamo Ijumaa katika robo fainali ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025. Matumaini ya Mali yalipata pigo kubwa katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza, wakati Yves Bissouma alipotolewa nje baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

 Samia aipongeza CAF kwa kuituza Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemshukuru Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe, kwa kutoa tuzo ya kutambua mchango wa Serikali ya Tanzania katika kukuza kandanda barani Afrika. Akizungumza katika Ikulu ya Dar es Salaam wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima ya wanamichezo wote waliofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, Januari 10, Rais Samia alisema jitihada, nidhamu na mshikamano uliooneshwa na wanamichezo hao ni alama ya uzalendo wa kweli na umeiwezesha Tanzania kupeperusha vyema bendera ya Taifa na kuandika historia mpya katika ulimwengu wa michezo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan

 

Amesema kuwa Tanzania inapoelekea kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, jukumu lililopo mbele ya Taifa ni kubwa na linahitaji mshikamano wa kitaifa, maandalizi ya mapema pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa michezo. Aidha, amebainisha kuwa ni wajibu wa Watanzania wote kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa heshima na manufaa ya Taifa, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji wazawa kwa kuwapa nafasi ya kucheza mechi nyingi za ndani ili kupata uzoefu, ushindani wa kutosha na maendeleo ya kitaaluma na kijamii.

Riadha: Kenya yang'ara Mbio za Dunia za Tallahassee

Rais William Ruto amewapongeza wanariadha wa Kenya kwa kufanya vyema katika Mashindano ya Dunia ya Riadha ya Tallahassee 26, akisifu ubabe na umbuji wao katika jukwaa la kimataifa. Kenya iliibuka kidedea katika mbio za wanaume wenye chini ya miaka 20, na kuzoa nafasi zote tatu za kwanza. Frankline Kibet alitwaa medali ya dhahabu, huku Emmanuel Kiprono akimaliza wa pili na kutwaa fedha, na Andrew Alamasi alimaliza wa tatu na kutia kibindoni medali ya shaba. Andrew Kiptoo alimaliza katika nafasi ya nne. Ruto amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Tunasherehekea ushindi mnono katika fainali ya U20 kwa wanaume, huku Frankline Kibet akitwaa dhahabu, Emmanuel Kiprono akishinda fedha, na Andrew Alamasi akipata shaba.

Wanariadha wa Kenya wang'ara Mashindano ya Dunia ya Riadha ya Tallahassee 26

 

Rais Ruto pia amempongeza Agnes Ngetich kwa ushindi wa kihistoria katika mbio za wanawake. Ngetich, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 10, aling'ara na kushinda taji la mbio za nyika kwa wanawake, na kuendeleza ubabe wa Kenya katika mashindano hayo. Alivuka mstari wa kumaliza kwa sekunde 42 mbele ya uwanja wote, na kuihakikishia Kenya taji la kumi mfululizo. "Tunampigia saluti Agnes Ngetich kwa ushindi mwingine wa kihistoria," Ruto alisema. Kwa upande wa wanaume, Mganda Jacob Kiplimo kwa mara ya tatu mfululizo aliibuka kidedea na kutwaa medali ya dhahabu, akimpiku Aregare wa Ethiopia na Mkenya Daniel Ebenyo aliyefunga orodha ya tatu bora na kutunukiwa medali ya shaba.

Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Barcelona imehifadhi taji la Kombe la Super la Uhispania (Spanish Super Cup) baada ya kuichabanga Real Madrid mabao 3-2 katika debi la ndovu kumla mwanawe la El Clasico lililopigwa Jumapili nchini Saudi Arabia. Baada ya Raphinha kuipeleka Barcelona mbele, Vinicius Junior aliisawazishia Madrid bao la kwanza kwa bao la kibinafsi na kuanza kipindi cha kwanza cha mchezo huko Jeddah. Lewandowski aliwarudisha Barca mbele, lakini Gonzalo Garcia alifunga bao la ziada dakika za mwisho na kuzifanya timu hizo kusawazisha wakati wa mapumziko. Mpambano huo uliamuliwa na bao la Raphinha lililopigwa baada ya dakika 73, huku Barca ikitwaa kombe la nne la utawala wa kocha Hansi Flick.

Mashabiki wa Barcelona wakisherehekea ushindi

 

Mwenzake wa Madrid, Xabi Alonso, alianza na nyota wa Ufaransa Kylian Mbappe kwenye benchi baada ya kukosa ushindi wa nusu fainali dhidi ya Atletico kutokana na jeraha la goti. Raphinha alifunga mara mbili kwa ajili ya Catalans siku ya Jumapili, huku Robert Lewandowski pia akiwa amefunga walipowashinda timu ya Xabi Alonso kwa ushindi wa 16 ulioweka rekodi, licha ya kadi nyekundu ya Frenkie de Jong. Barca walianza kuongeza joto kwa Madrid, na Raphinha akapata bao la kufutia machozi baada ya dakika 36. Haikushangaza kwamba baada ya kufunga bao la kwanza na la ushindi, Raphinha wa Barcelona anapewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.

Mbali na hayo, klabu za Arsenal na Liverpool zilitoshana nguvu katika mchuano wa watu wazima wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Arsenal walipoteza nafasi ya kusonga mbele kwa tofauti ya pointi nane kileleni mwa EPL, ilipolazimishwa sare tasa na Liverpool kwenye Uwanja wa Emirates. Wekundu hao ni moja kati ya timu mbili pekee zilizowashinda vijana wa Mikel Arteta msimu huu, na walikaribia kuvunja uzio Alkhamisi wakati Conor Bradley alipogonga mwamba wa goli. Arsenal wanasalia kileleni mwa jedwali la EPL wakiwa na alama 49 huku Liverpool wakiwa katika nafasi ya nne kwa alama 35. Katika mechi nyingine za EPL, New Castle iliizaba Leeds mabao 4-3 Jumatano, siku ambayo Manchester United 'Mashetani Wekundu' walikuwa wanalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Burnley. Mancester City ambao wapo katika nafasi ya pili ligini wakiwa na alama 43, walihemeshwa na Brighton na mchuano wao ukaishiakwa sare ya bao 1-1.  City wana pointi sawa na Aston Villa wanaofunga orodha ya tatu bora kwa sasa, baada ya kulazimishwa sare tasa na Crystal Palace. Tusubiri Jumamosi tuone nani zaidi, kati ya Man City na Man United katika ngoma nyingine ya aina yake.

Na klabu ya Nottingham Forest imeonyesha nia ya kumsajili mchezaji wa kimataifa wa Iran, Mehdi Taremi. Taremi amefunga mabao 11 na kutoa pasi mbili za mabao katika mechi 19 kwa Olympiacos, idadi ambayo imevutia klabu hiyo ya Uingereza.

Nyota wa soka wa kimataifa wa Iran,  Mehdi Taremi

 

Nottingham Forest, ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya 17 katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, itaimarisha safu yake ya ushambuliaji iwapo itamsajili mshambuliaji huyo. Taremi ambaye amewahi kukipiga Porto na Inter Milan, anaweza kusainiwa rasmi wakati litakapofunguliwa dirisha la uhamisho.

.........................TAMATI................