Ulimwengu wa Spoti, Jan 19
Hujambo msikilizaji mpenzi, na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku zilizopita, ikiwemo fainali ya michuano ya AFCON. Nakusihi tuwe sote hadi tamati ya kipindi…..Karibu…….
MMA: Iran mshindi wa 2 Japan
Timu ya Taifa ya Shirikisho la Sanaa Mseto ya Kijeshi (Mixed Martial Arts) ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika Michezo ya Asia huko Nagoya, Japan. Kwa kuzoa medali 14, wanamichezo wa MMA wa Iran wamezoa alama nane katika Michezo ya Asia. Kikosi cha Iran kilichojumuisha wanamichezo 13 wa kiume na saba wa kike kiling'ara na kuipaisha bendera ya Iran katika mashindano hayo ya kibara. Moslem Fathollahi na Sajjad Azizi walinyakua medali za dhahabu. Fatemeh Akhlaghizadeh, Mobina Amiri, Ali Shadman, Ali Akbar Ahmadi, Mohammad Reza Sadeghi na Hadi Abbasi walizawadiwa medali za fedha.

Hasti Sadat Mir, Faezeh Eslamipour, Kamand Deh-Pahlavan, Amir Mohammad Hadi Hamid, Ali Akbar Taleshi na Mohammad Jalilzadeh walinyakua medali za shaba. Mixed Martial Arts ni mchezo unaojumuisha mbinu za michezo mbalimbali ya mapigano kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu. Kimsingi, mchezo huo wa sanaa una mchanganyiko wa mbinu na sanaa tofauti kutoka pembe tofauti za dunia, kama vile Muay Thai, Kyokushin, ndondi, kickboxing, taekwondo, wushu sanda (ndondi ya Kichina), judo, jujitsu ya Brazil na mieleka.
Ukweaji Barafu; Iran yazoa medali
Wakweaji barafu wawili wa Iran wamefanikiwa kushinda medali ya dhahabu na shaba katika fainali za Kombe la Dunia 2026 zilizoandaliwa na Shirikisho la UIAA nchini Korea Kusini. Wakati wa raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia la Kupanda Barafu la UIAA la 2026 huko Cheung-Sung, Korea Kusini, Mohammad-Reza Safdarian alinyakua medali ya dhahabu na Mohsen Beheshti akatwaa medali ya shaba. Wanamichezo hao wa Iran walifuatwa na mwanichezo kutoka Mongolia.

Mkweaji barafu wa kike wa Iran Mahin Khalili alishika nafasi ya tano katika mashindano haya katika daraja la kasi. Raundi ya pili ya fainali za Kombe la Dunia la Kukwea Barafu la UIAA imepangwa kufanyika Uswisi katika wiki ya mwisho ya mwezi huu wa Januari.
AFCON: Senegal yaibuka kidedea
Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025 imefikia tamati, kwa kuibuka kidedea Senegal. Simba wa Teranga wametwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika mchezo wa fainali uliopigwa Jumapili usiku wa Januari 18, huko Rabat, mji mkuu wa Morocco. Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa huku timu zote zikionesha kiwango cha juu, jambo lililosababisha dakika 90 za kawaida kumalizika bila mshindi, na kulazimika kuongezwa dakika 30 za muda wa nyongeza.

Baadhi ya wachambuzi wa spoti wanadai kwamba, kumekuwepo na njama mbali mbali za kuwabeba wenyeji tangu mwanzoni mwa mashindnao hayo ya kibara, ikiwemo penati waliotunikiwa Waarabu hao wa kaskazini mwa Afrika katika fainali ya Jumapili. Dakika ya 107 ya mchezo huo, mshambuliaji wa Senegal, Pape Alassane Gueye alipachika bao la pekee lililoihakikishia Senegal ushindi na hatimaye kutwaa taji la AFCON kwa mara ya pili katika historia ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Morocco ilitinga fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuitoa Nigeria katika mchezo wa nusu fainali kwa kuibinjua mabao 4-2 kwenye upigaji penati. Senegal nayo ilifuzu fainali kwa kuitandika Misri bao 1-0 katika mchezo mwingine wa nusu fainali. Senegal sasa imeishinda Morocco kwa mara ya pili katika Kombe la Mataifa ya Afrika - lakini ni baada ya fainali hiyo ya Jumapili kugubikwa na suitafahamu na vuta nikuvute, wakati ambapo Lions of Teranga walipokataa kuendelea na mchezo kwa muda, wakati wenyeji walipopewa penalti tata ya dakika za mwisho huku mechi ikiwa bila bao. Bingwa Senegal imetunukiwa zawadi ya dola milioni 10 za Kimarekani, hilo likiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na mwaka 2023. Mshindi wa pili, Morocco amepokea dola milioni 4, kama ilivyotangazwa na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika CAF Patrice Motsepe, kwa ajili ya kuongeza motisha na ushindani kwenye fainali hizo. Morocco sasa imepoteza fainali ya pili baada ya kupoteza ile ya mwaka 2004 dhidi ya Tunisia.
Katika hatua nyingine, kipa Stanley Nwabali aliokoa penalti mbili ikiwemo ya kwanza kutoka kwa Mohamed Salah na kuifanya Nigeria kuishinda Misri kwa mabao 4-2 katika upigaji matuta, na kushinda medali ya shaba katika mechi ya Jumamosi ya kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la Mataifa ya Afrika. Ademola Lookman alifunga penalti ya ushindi katika mechi hiyo ya kusisimua.
Mikwaju ya Salah na Omar Marmoush iliokolewa na Nwabali baada ya timu hizo kutoka sare ya 0-0 katika muda wa kawaida. Ulikuwa upigaji penalti wa pili mfululizo kwa Super Eagles kufuatia sare ya bila kufungana baada ya kupoteza nusu fainali dhidi ya Morocco siku ya Jumatano. Super Eagles walimaliza Kombe la Afrika wakiwa katika hali na mkondo mzuri, tofauti na duru iliyopita ya AFCON, ambapo walipoteza katika fainali dhidi ya mwenyeji Ivory Coast.
Soka Tanzania; Ulipo Tupo Bingwa Super Cup
Klabu ya kandanda ya Ulipo Tupo Lake Zone imetwaa ubingwa wa soka wa CRDB Super Cup ya Tanzania msimu wa tano, baada ya kuifunga timu ya Wakala Central Zone goli 1-0 katika mchezo wa fainali uliokuwa na ushindani mkubwa, uliopigwa katika Uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha. Kwa matokeo hayo, timu ya Ulipo Tupo ilifanikiwa kupata zawadi ya kitita cha fedha taslimu Shilingi milioni 15 na kikombe, ambapo kwa upande wa mpira wa pete, mvutano ulikuwa mkubwa kati ya timu vya Ulipo Tupo Queens na timu ya Popote Inatiki Queens, ambapo Ulipo Tupo Queens Central Zone iliibuka mshindi wa jumla ya magoli 40 kwa 30 na kujinyakulia zawadi ya Shilingi milioni 11 za Tanzania fedha taslimu. Akizungumza baada ya fainali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amosi Makallah, amesema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kukuza uchumi wa Mkoa huo na sehemu ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo itaendelea kuwekeza kwenye michezo kwa maendeleo ya jamii, na kuhimiza michezo kazini na kujenga afya ili kuondokana na magonjwa nyemelezi ambayo, kufanya mazoezi ni moja ya kinga kubwa.
Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kufanikisha ujenzi wa viwanja vya michezo katika kila Wilaya, pamoja na ujenzi wa Viwanja vya Mikoa kwa Unguja na Pemba. Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo 13 Januari 13, katika Uwanja wa Michezo wa Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati wa uzinduzi rasmi wa uwanja huo uliokwenda sambamba na mchezo wa fainali ya Michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Azam FC na Yanga SC za Dar es Salaam.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewashukuru wadhamini wote wa Michuano ya Kombe la Mapinduzi, kwa kufanikisha mashindano hayo maalum yanayolenga kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar na kuendeleza michezo, hususan soka. Katika mchezo huo wa fainali, klabu ya Yanga African imefanikiwa kulitwaa Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5–4 dhidi ya Azam FC, kufuatia timu hizo kutoka sare ndani ya dakika tisini za mchezo. Yanga SC ilizawadiwa Shilingi Milioni 150 za Ubingwa pamoja na Kombe la Mapinduzi, tuzo iliyokabidhiwa na Rais Mwinyi.
Riadha: Kenya yawika Ulaya na Asia
Mwanariadha nyota wa Kenya, Brian Kibor ameendelea kudhihirisha umahiri wake katika mbio za barabarani baada ya kuibuka kidedea katika mbio za Santa Pola Nusu Marathoni nchini Uhispania siku ya Jumapili, akiongoza kikosi cha wanaume Wakenya waliotwaa nafasi tatu za kwanza. Kibor alishinda kwa kutumia dakika 1:00:49, akimpiku mwenzake Simon Maywa, ambaye alitumia dakika 1:02:59 kwa nafasi ya pili, huku Kipkandie Mkulia akikamilisha ushindi wa tatu bora wa Kenya kwa dakika 1:03:03. Katika mbio za wanawake huko Santa Pola, Daisilah Jerono wa Kenya alishinda mbio hizo kwa utulivu na kuchukua heshima za juu kwa muda wa 1:07:27. Esther Chebet wa Uganda alishinda nafasi ya pili kwa muda wa 1:08:13, huku Hanna Lindholm wa Sweden akikamilisha jukwaa kwa muda wa 1:12:03.
Kwingineko mwanariadha bingwa wa Kenya, Vincent Kipchumba siku ya Jumapili aliendeleza fomu nzuri ya kukimbia barabarani kwa Kenya kwa kushinda Montferland Half Marathon nchini Uholanzi, akitumia 1:01:39. Mkenya Silas Kiprono (2:09:56) na Francis Langat (2:09:59) waliambulia nafasi ya pili na ya tatu mtawalia, wakimaliza tu nyuma ya Melaku Bizuneh wa Ethiopia, aliyeshinda kwa saa 2:09:3 Katika mbio za wanawake, Linet Masai alimaliza wa tatu kwa saa 2:29:23, nyuma ya Shitaye Eshete wa Bahrain (2:27:03) na Nigisti Tesfay wa Ethiopia (2:29:13). Wanariadha wa Kenya na Ethiopia waling'ara pia katika mbio za Marathon za Mumbai.
Ligi ya EPL
Michael Carrick ameanza vyema kama meneja wa muda wa Manchester United kwa ushindi mkubwa wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City katika debi la Manchester, kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Akichukua jukumu la mchezo wake wa kwanza tangu kuteuliwa kwake hivi karibuni, Carrick mara moja aliondoa giza lililokuwa limetanda Old Trafford kwa ushindi wa kishindo wa Jumamosi ambao huenda ukadumu kwa muda mrefu katika kumbukumbu za mashabiki wa Mashetani Wekundu.
Kiungo huyo wa zamani wa United amesaini mkataba hadi mwisho wa msimu na ana michezo 17 ya kuwashawishi uongozi wa klabu hiyo kumpa kazi hiyo ya kudumu baada ya Ruben Amorim kufukuzwa kazi wiki iliyopita. Carrick hangeweza kutoa taswira nzuri zaidi ya kwanza kwa utendaji mzuri dhidi ya meneja wa City Pep Guardiola katika debi ya 198 ya Manchester. Mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Bryan Mbeumo na Patrick Dorgu yalifunga ushindi ambao uliwafanya mashabiki wa United kuimba kwa sauti kamili na kuwazima wapinzani wao wakali wa jiji.
Katika mechi nyingine za karibuni za EPL, vigogo waliotuama kileleni, Arsenal ililazimishwa sare tasa na Nottingham Forest wakati ambapo Villa alikuwa anapokezwa kichapo laini cha bao 1-0 na Everton. Liverpool pia ilibanwa koo na Burnley na mchuano huo wa wikendi ukaishia kwa sare ya bao 1-1. Waliovuna ni Chelse ambao waliichabanga Brentford mabao 2-0. Gunners wanasalilia kileleni kwa jedwali la EPL wakiwa na alama 50, alama saba zaidi ya City na Villa ambao kwa sasa wanaridhika na nafasi na ya pili kwa usanjari huo. Liverpool wapo katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 36, alama moja zaidi ya Man U wanaofunga orodha ta 5 bora kwa sasa.
..........................TAMATI.................