Kan'ani: Tuzo ya Amani ya Nobel inatolewa kisiasa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa hatua ya waandaaji wa Tuzo ya Amani ya Nobel kumpa tuzo hiyo mwanamke wa Kiirani ambaye ameshitakiwa mara kadhaa kwa kufanya vitendo vya jinai hapa nchini.
Katika taarifa, Nasser Kan'ani amesema kitendo hicho cha kuchukiza cha Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huu 2023 kutunukiwa mwanamke huyo wa Kiirani mwenye faili jeusi la jinai kimefanyika kisiasa.
Kan'ani amebainisha kuwa, "Hatua ya kisiasa ya Kamati ya Tuzo ya Nobel inaenda sambamba na sera za baadhi ya nchi za Ulaya za uingiliaji na zilizo dhidi ya Iran."
Aidha Kan'ani ameikosoa Kamati ya Nobel kwa kutoa madai ya urongo na yasiyo na msingi wowote juu ya matukio ya hapa nchini Iran akieleza kuwa, uropokaji huo wa baadhi ya madola ya Ulaya unakusudia kupotosha ukweli wa mambo na kufifiza hatua za ustawi zilizopigwa hapa nchini.
Jana Ijumaa na katika hatua ya kisiasa, Kamati ya Tuzo ya Nobel yenye makao yake nchini Norway, ilimtunuku Narges Mohammadi (51) Tuzo ya Amani ya Nobel mjini Oslo, ikidai kuwa mwanamke huyo wa Kiirani amekuwa mstari wa mbele kupambana na dhulma dhidi ya wanawake wa Kiirani, na eti ni mtetezi wa haki za binadamu na uhuru kwa watu wote.
Hii ni katika hali ambayo, mwanamke huyo katika katika kipindi karibu chote cha utu uzima wake amekuwa akikamatwa na kufungwa jela kwa makosa ya jinai, na hivi sasa pia anatumikia kifungo katika Gereza la Evin hapa Tehran.
Huko nyuma pia, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni unaoua watoto Wapalestina, na Mohammad bin Zayed al Nahyan, mrithi wa ufalme wa Imarati ambaye mikono yake imetapakaa damu za maelfu ya Wayemen, walipendekezwa na mshindi mmoja wa tuzo ya Nobel kutunukiwa tuzo hiyo ya amani.